Valentine Obara: Aga Khan ‘imenilea’ tangu kuzaliwa hadi kuajiriwa
KATIKA mwaka wa 1992, nilipata fursa ya kufanya majaribio ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Aga Khan mjini Mombasa.
Kabla ya hapo, uhusiano wangu na taasisi za Aga Khan ulikuwa tayari umeanza miaka michache awali nilipozaliwa katika Hospitali ya Aga Khan iliyo mjini humo.
Hata hivyo, matamanio yangu kujiunga na Shule ya Msingi ya Aga Khan Januari 1993 hayakufua dafu kwa sababu ya wingi wa wanafunzi. Kwa wema wao, wasimamizi wa shule hiyo wakanitafutia nafasi katika shule mbadala iliyokuwa ya viwango sawa.
Miaka tisa baadaye, kama kwamba nyota ya maisha yangu ilinuia niwe katika mazingara ya shule za Aga Khan, nilipokea barua kutoka kwa Wizara ya Elimu kujiunga na Shule ya Upili ya Aga Khan baada ya matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi kutolewa.
Shule hiyo, ile ya msingi na chekechea zote ziko ndani ya kiwanja kimoja katika eneo la Kizingo.
Wakati huo, Shule ya Upili ya Aga Khan ilikuwa katika ngazi ya shule za mikoa. Shule za upili zilikuwa zimegawanywa kwa ngazi za kitaifa, mikoa na wilaya.
Hapo ndipo nilishuhudia jinsi Aga Khan alivyoenzi uwekezaji katika elimu bora.
Kutoka kwa maabara yenye vifaa vyote vya elimu za sayansi, maktaba iliyojaa vitabu muhimu sio tu kwa mafunzo ya darasani bali pia vya kujielimisha kuhusu mambo mengi zaidi ya kimaisha, maabara ya mafunzo ya tarakilishi miongoni mwa mengine, shule hii ilikuwa ya kuvutia kwa yeyote mwenye ari ya kukata kiu ya elimu.
Muundo wa shule ulikuwa salama kwa kila mmoja, rasilimali za michezo ikiwemo uwanja mkubwa na kidimbwi cha uogeleaji pamoja na usafi wa hali ya juu yaliwapa wanafunzi mazingira bora.
Sawa na wenzangu wengi katika shule hiyo, nilifanikiwa kukamilisha Kidato cha Nne nikajiunga na Chuo Kikuu cha Maseno kusomea uanahabari.
Mapenzi yangu ya lugha na uandishi yalidhihirika, na kwa kuongezea mafunzo ya uanahabari niliyopokea, nilikuwa mmoja wa wanafunzi watatu wa Maseno waliopewa nafasi kufanya mafunzo kwa vitendo katika kampuni ya Nation Media Group, tawi la Kisumu.
Hii ilikuwa nafasi yangu, kwa mara ya tatu, kuwa na uhusiano wa karibu na shirika la Aga Khan.
Kampuni hii iliniajiri punde baada ya kukamilisha muda wa mafunzo kwa vitendo na tangu wakati huo, nimepata fursa ya kuchangia na kusimamia uanahabari wa hali ya juu unaosifiwa kote ulimwenguni.
Kando na haya, kazi ya uanahabari katika Nation Media Group pia imenipa nafasi ya kupokea mafunzo mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Aga Khan jijini Nairobi mara kadhaa.
Bila shaka, Aga Khan ameacha sifa kubwa katika kila sekta aliyowekeza, na nimebahatika kuwa mmoja wa Wakenya waliopata fursa ya kunufaika na mchango wake moja kwa moja.
Mwandishi ni Mhariri wa Eneo la Pwani, Nation Media Group