UDA yatuma maafisa kwenda kupata ‘mafunzo’ kutoka NRM ya Museveni
CHAMA tawala cha United Democratic Alliance (UDA), ambacho kiongozi wake ni Rais William Ruto, kimetuma ujumbe wa maafisa wakuu 19 kushauriana na National Resistance Movement (NRM) kinachotawala Uganda cha Rais Yoweri Museveni.
Ujumbe wa UDA unaongozwa na Katibu Mkuu Hassan Omar huku Rais Ruto akilenga kupata mafunzo kutoka kwa NRM ambacho kimekuwa mamlakani tangu 1986.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, UDA ilisema Bw Omar aliongoza wajumbe kutoka makao makuu ya chama kuzuru Taasisi ya Uongozi ya NRM kwa zoezi la kujifunza.
“Timu hiyo ilikaribishwa kwa moyo mkunjufu na Mkurugenzi wa Taasisi, Kanali Okei Rukogota, ambaye aliwapa maelezo ya mtaala wa taasisi hiyo.
Kanali Rukogota alisisitiza kuwa Taasisi ya Uongozi ya NRM ni kituo cha ubora kinachojitolea kutoa viongozi wenye ujuzi na maono waliojitolea kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi nchini humo,” ilisema taarifa ya UDA.
Bw Omar aliandamana na Mweka Hazina wa Kitaifa Japheth Nyakundi, Mkurugenzi Mkuu Nicodemus Bore, na wanachama wengine wa kitaifa.
Bw Omar alifichua nia ya UDA ya kuanzisha taasisi kama hiyo huku akisisitiza umuhimu wa kujifunza kutoka kwa muundo wa NRM.
NRM kwenye tovuti yake ilisema ujumbe wa UDA ulipokewa na Katibu Mkuu wa NRM, Richard Todwong na Mkurugenzi wa Masuala ya Nje Meja (mstaafu) Awich Pollar.
Bw Todwong alisema NRM na UDA zinatazamia kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na ushirikiano wa kimkakati kati ya vyama hivyo viwili vya kisiasa.
Ujumbe huo wa UDA uliwasili Uganda Jumanne na unatarajiwa kushiriki shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukutana na Rais Museveni, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitaifa wa NRM.
NRM ilianzishwa kama vuguvugu la ukombozi ambalo liliendesha mapambano ya muda mrefu dhidi ya tawala zilizotangulia. Katika tovuti yake, NRM inadai kuwa imerejesha utulivu wa kisiasa, heshima kwa haki za binadamu, umoja wa kitaifa, amani, usalama na utawala wa sheria.
Pia inajigamba kuwa imeanzisha demokrasia na kurejesha uchaguzi huru na wa haki.
Hata hivyo, wakosoaji wanalalamikia kuzimwa kwa demokrasia na utawala wa NRM. Watu wanaochukuliwa kuwa wakosoaji wa Rais Museveni wamekuwa wakikamatwa na kuzuiliwa kiholela. Madai ya kuvuruga uchaguzi ni kawaida nchini Uganda chini ya utawala wa miaka 39 wa Museveni
UDA pia imekuwa ikishirikisha Chama cha Kikomunisti cha China.
Mnamo 2024, maafisa wa UDA walishauriana na Chama cha Kikomunisti cha China.
Katika mazungumzo yake, UDA ilitaka ufadhili wa Sh1 bilioni kutoka kwa chama hicho cha China kusaidia shughuli zake za kisiasa.
UDA pia ilitaka kuungwa mkono na chama hicho ili kujenga makao yake rasmi na ya kudumu kwenye ardhi ambayo tayari kimepata jijini Nairobi