Utata kuhusu shughuli za serikali bungeni baada ya Kenya Kwanza kupokonywa taji
SHUGHULI za serikali katika Bunge la Kitaifa huenda zikaathiriwa kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kuupokonya mrengo wa Kenya Kwanza hadhi ya kuwa muungano wa walio wengi katika bunge hilo endapo uamuzi huo hautabatilishwa na Mahakama ya Rufaa.
Japo mahakama hiyo haikusema ni lini uamuzi huo utaanza kutekelezwa, mawakili Charles Kanjama na David Ochami wanasema unapasa kutekelezwa mara moja.
Hii ndio maana punde uamuzi huo ulipotolewa Bunge la Kitaifa liliomba utekelezwe baada ya siku 45, ombi ambalo majaji walikataa.
“Kutakuwa na mabadiliko kadhaa endapo Spika hatapokea maagizo kutoka Mahakama ya Rufaa ya kusitisha utekelezaji wa uamuzi huo,” akasema Bw Kanjama ambaye ni Wakili Mkuu.
“Kiongozi wa wengi ndiye, kawaida, huwasilisha ajenda za serikali bungeni na hili halitawezekana kufuatia uamuzi huo wa mahakama uliotolewa Ijumaa wiki jana,” akaongeza Bw Kanjama.
Wabunge wanaporejelea vikao vya kawaida Jumanne Februari 11, Taarifa ya Sera Kuhusu Bajeti (BPS) inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa na Hazina ya Kitaifa.
Taarifa hiyo inapasa kuwasilishwa kabla ya Februari 14, 2025, kulingana na hitaji la Sheria kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma ya 2012.
Kulingana na sheria hiyo siku ya mwisho kwa BPS kuwasilishwa katika bunge la kitaifa ni Februari 15, kila mwaka.
Kwa kuwa Februari 15 mwaka huu ni Ijumaa, siku ambayo bunge huwa haliendeshi vikao, BPS inatarajiwa kuwasilisha siku moja kabla, Alhamisi Februari 14, kazi ambayo inapasa kufanywa na kiongozi wa wengi.
Kwa sababu chini ya mfumo wa urais bunge linatarajiwa kufanyakazi pamoja, ajenda za serikali huwasilishwa na kiongozi wa walio wengi na kuungwa mkono na mbunge kutoka mrengo wa walio wachache.
Japo uamuzi wa mahakama haujafutilia mbali ukweli kwamba chama cha UDA chake Rais William Ruto ndicho chenye idadi kubwa ya wabunge, umeiupa muungano wa Azimio hadhi ya muungano wa walio wengi.
Hii ina maana kuwa muungano huo ndio unapaswa kuwa na idadi kubwa ya wanachama katika kamati za bunge zinazopiga msasa utendakazi wa wizara za serikali.
Tofauti ya kipekee ni uaminifu wa wabunge waliochaguliwa kwa tiketi za vyama ambavyo vilijitenga na Azimio japo hatua hiyo haukufanywa kisheria.
Vyama hivyo ni kama vile United Democratic Movement (UDM), Movement for Democracy and Growth (MDG), Maendeleo Chap Chap (MCC), Chama cha Mashinani (CCM) na Pamoja African Alliance (PAA).
Uaminifu wa wabunge 14 kutoka vya hivi vitano hautabadilishwa na uamuzi huo wa mahakama kuu uliotolewa Ijumaa.