Dimba

Blues wala kirungu FA ikichacha

Na MASHIRIKA February 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, UINGEREZA

MATUMAINI ya Chelsea kutwaa taji msimu huu yalididimia baada ya kupepetwa 2-1 na wenyeji Brighton & Hove Albion katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Uingereza (FA Cup) uwanjani Amex, Jumamosi usiku.

Brighton itaungana na Manchester City, Newcastle, Cardiff City, Bournemouth, Fulham na Burnley ambazo pia zilizoa ushindi Jumamosi na kutinga raundi ya tano ya kombe hilo la jadi kabisa katika soka ya Uingereza. Manchester United ilifuzu awali Ijumaa.

Mnamo Jumamosi, Blues walibanduliwa licha ya kuchukua uongozi wa mapema baada ya kipa wa Brighton kujifunga.

Masogora wa kocha Enzo Maresca walikuwa butu katika mashambulizi licha ya kuweka kikosi imara uwanjani kilichojumuisha mastaa Cole Palmer, Jadon Sancho, Enzo Fernandez na Moises Caicedo.

Walituma makombora saba usiku mzima huku moja pekee likilenga shabaha – makombora mawili yakiwadia kabla ya goli hilo la mapema lililofungwa dakika ya tano.

Krosi ya Cole Palmer ilitumbukizwa wavuni na kipa Bart Verbruggen. Hata hivyo, Blues walikuwa kifua mbele dakika chache tu huku goli hilo la kismati likiwa shambulizi pekee la maana ambalo walifanya usiku kucha.

Brighton ya kocha Fabian Hurzeler walisawazisha muda mfupi baadaye kupitia hedi ya Georginio Rutter dakika ya 12 alipounganisha krosi ya Joel Veltman.

Chelsea walitapata bila makali yoyote na katika kipindi cha pili Rutter aliwaadhibu tena alipomuandalia Kauro Mitoma pasi murwa aliyoiinua juu ya kipa Robert Sanchez na kumimina wavuni bao la ushindi dakika ya 57.

Maresca alifanya mabadiliko lakini hayakuzaa matunda.

Sasa Chelsea wataelekeza juhudi zao kwa Ligi Kuu (EPL), ambako wanashikilia nafasi ya sita, na wamekuwa wakisuasua, pamoja na kipute cha Uefa Conference League ambacho itawalazimu kushinda kwani sasa ndiyo fursa ya pekee ya hakika kwao kurejea katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Leo usiku itakuwa zamu ya Crystal Palace kuruka kamba ya wenyeji Doncaster Rovers – inayoshiriki ligi ya daraja ya chini EFL League Two – katika uwanja wa Eco-Power.