Jamvi La Siasa

Jinsi vita baridi vya Uhuru, Gachagua vyaweza kumrudisha Ruto Ikulu bila kijasho

Na MWANGI MUIRURI February 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUENDA ushindani unaohusu ni nani ateuliwe kuwania urais kati ya Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i ukahujumu juhudi za upinzani kuunda muungano thabiti wa kuzima nia ya Rais William Ruto kushinda tena uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027.

Tofauti hizi pia zimechipuka katika ukanda wa Mlima Kenya ambapo mrengo wa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua unaonekana kumchangamkia Bw Musyoka naye Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akionekana kuchangamkia wazo la Dkt Matiang’i kupeperusha bendera ya upinzani katika uchaguzi huo ujao.

Jumapili, katika mahojiano na wanahabari wa vituo vinavyotangaza kwa lugha ya Kikuyu, Bw Gachagua alipuuzilia mbali chama cha Jubilee na kukitaja kama “Wilbaro nyekundu”, ishara kuwa anapinga juhudi za chama hicho kinachoongozwa na Bw Uhuru kuunga Dkt Matiang’i, ambaye Bw Gachagua amewahi kudai alitumia vyombo vya usalama kumnyanyasa katika uchaguzi mkuu uliopita.

Bw Gachagua alionekana kufananisha chama hicho na Wilbaro ya manjano, alama ya chama tawala cha UDA, chake Rais Ruto. Aliapa kuongoza wafuasi wake kutoka Mlima Kenya kugura UDA na kujiunga na chama kipya ambacho atakitaja Mei mwaka huu.

“Hizo wilbaro sharti zishutumiwe na watu wetu wahamasishwe ili wajue wadhamini wanaolenga kugawanya Mlima,” Bw Gachagua akasema.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni aliambia Taifa Leo kwamba “kuna mgawanyiko mkubwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa kutoka Mlima Kenya” kwa sababu kila mmoja anavuta upande wake.

“Tumekuwa tukiendeleza ajenda ya Matiang’i kutokana na sababu kadhaa ambazo hazifai kukutia wasiwasi. Kama chama tunaamini kuwa unaweza tu kusaka wafuasi vizuri ikiwa una mgombeaji wa urais,” Bw Kioni akasema.

Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragwa alisema “kutaja Dkt Matiang’i hakumaanishi kuwa tumeamua kushirikiana naye’,’ kauli ambayo alionekana kuitumia kumjibu Bw Gachagua.

“Ni mgombeaji wetu na tuko tayari kuendelea kufanya mazungumzo huku tukiimarisha chama chetu,” akasema Bw Kioni.
Bw Kioni aliongeza kuwa “japo kuna tofauti hapa na pale, tumeungana katika ajenda moja ya kumwondoa mamlakani Dkt Ruto 2027 licha ya kwamba kuna watu fulani wanaotaka kumhujumu Bw Kenyatta na kumpokonya chama cha Jubilee”.

Alikuwa akirejelea kundi la viongozi wa Jubilee wakiongozwa na Mbunge Maalum Sabina Chege waliojaribu kuchukua udhibiti wa Jubilee kutokana na usaidizi wa mrengo wa Rais Ruto.

Hata hivyo, Bw Kioni alisema wao kama wanachama wa Jubilee wako radhi kushirikiana na Bw Gachagua kwani ni “mmoja wa mashujaa wanaoweza kumpiga vita Rais Ruto”.

“Kile tunachotaka ni sote kushirikiane kwa nia njema na kuendelea kama kikosi kimoja pasi watu fulani kuanza kutuamurisha baadhi yetu,” akasema Bw Kioni.

Kulingana na Katibu huyo Mkuu wa Jubilee, Rais Kenyatta anasalia kuwa msemaji wa Mlima Kenya ambaye pia anafaa kutoa ushauri kuhusu mkondo wa kisiasa ambao eneo hilo linapaswa kufuata.

“Kumbuka Bw Kenyatta alikuwa ametuonya kwamba tulikuwa tukielekea pabaya kwa kumuunga mkono Bw Ruto. Sasa sote, akiwemo Gachagua, tunakubaliana kwamba alikuwa anasema ukweli. Tunapoelekea 2027 tunapaswa kuongozwa na hekima ili tusirudie kosa tulilofanya 2022,” akasema.

Zamani, Bw Gachagua alikuwa msaidizi wa Bw Kenyatta, wakati wote walikuwa wanachama wa Kanu na wakaungana tena kati ya 2017 na 2022 ambapo Bw Kenyatta alikuwa Rais na Gachagua akihudumu kama Mbunge wa Mathira kwa tiketi ya chama cha Jubilee.

Lakini mahusiano yao yalivunjika nyakati za kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 walipounga mkono wagombeaji tofauti.

Bw Kenyatta alimtelekeza aliyekuwa naibu wake, Dkt Ruto, na kuunga mkono mgombeaji wa Azimio Raila Odinga huku Martha Karua akiwa mgombea mwenza.

Kwa upande wake, Dkt Ruto alimteua Gachagua kuwa mgombea mwenza wake na wakaibuka washindi.