Habari za Kitaifa

Simon Muteti aachiliwa huru miezi mitatu baada ya kutekwa nyara

Na STEVE OTIENO February 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIMON Muteti, ambaye inadaiwa alitekwa nyara na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi mnamo Oktoba mwaka jana huko Timau, kaunti ya Laikipia, amepatikana akiwa hai baada ya takriban miezi minne akitafutwa na marafiki na familia.

Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Faith Odhiambo alisema kuwa Bw Muteti ameunganishwa tena na familia yake.

Ingawa alifurahishwa na habari za kuachiliwa kwake, Bi Odhiambo alisema kuwa Bw Muteti ametishika sana na masaibu aliyopitia mikononi mwa watekaji nyara ambao LSK inadai ni maafisa wa Kitengo Maalum cha Operesheni huko Timau.

LSK  imesema itamsaidia mwathiriwa na familia yake kupata msaada wa kisheria na kisaikolojia.

“Simon Muteti ameachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu. Yuko salama na familia yake lakini bado ametishika kutokana na masaibu aliyopitia,” alisema.

Maelezo ya walioshuhudia kutekwa kwake yanaonyesha alitekwa nyara mnamo Oktoba 22, 2024, huko Timau, Kaunti ya Laikipia, na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa usalama wa serikali.

Kutekwa kwake kulitangazwa na LSK mnamo Januari 2025, baada ya familia yake kuomba chama usaidizi wa kisheria.

“Kisa hiki cha kutatanisha kinasisitiza hali ya kutisha ya kutekwa nyara na kutoweka kwa watu sio tu katika maeneo ya mijini kama Nairobi lakini kote nchini,” Bi Odhiambo alisema.

LSK ilifichua kuwa wakati  ambao kisa cha Bw Muteti  kiliripotiwa  kwake, familia nyingine kutoka Garsen, kaunti ya Tana River, pia ilitembelea afisi zake jijini Nairobi.

Familia hiyo, iliyowakilishwa na mwanamume aliyetambuliwa kama Ibrahim Abdullahi, iliripoti kwamba baba yao, Abdullahi Ahmed alipotea Oktoba 5, 2024.

Visa hivi vilisababisha LSK kuongeza juhudi zake za kutoa usaidizi wa kisheria, kukusanya taarifa, kusaidia familia zilizoathirika na kuongeza ufahamu, kupitia ushirikiano na mashirika mengine.

Kuachiliwa kwa Muteti kunajiri mwezi mmoja baada ya vijana watano waliokuwa wametekwa nyara Disemba mwaka jana kuachiliwa na watekaji wao.

Wanaume hao ni pamoja na Billy Mwangi, 24, Peter Muteti (22), Kibet Bull, Rony Kiplangat na Bernard Kavuli.

Bw Mwangi alisaidiwa na msamaria mwema akaungana na watu wa familia yake, Peter Muteti alipatikana akiwa hai katikati ya Nairobi.

Bw Kiplangat alipatikana Machakos, Kavuli akapatikana Kitale naye Bw Bull alipatikana Vihiga.

Tofauti na wanaume waliotajwa hapo awali waliorejea wakiwa hai baada ya kuzuiliwa na watekaji wao, miili ya wanaume wawili, Martin Mwau na Justus Mutumwa, waliotekwa nyara eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos Desemba mwaka jana, ilipatikana katika mochari ya kaunti ya Nairobi na kutambuliwa na familia zao.

Katika visa hivi vyote, familia za waathiriwa na mashahidi walioshuhudia wanasisitiza kuwa wote walitekwa nyara na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa usalama wa serikali.