Aliyesafiri kwa miadi ya Valentino mjini apatikana ameuawa kikatili
FAMILIA moja katika kijiji cha Kirima, Kaunti ya Kirinyaga, inaomboleza kifo cha binti yao, Risper Ng’endo, 26, aliyepatikana ameuawa kikatili, baada ya kualikuwa na mpenzi wake washerehekee siku ya wapendanao (Valentino).
Mnamo Februari 1, Ng’endo alienda jijini Nairobi kumuona mpenzi wake lakini hiyo ilikuwa mara ya mwisho familia yake kumuona akiwa hai.
Kulingana na familia hiyo, Ng’endo alipigiwa simu na mpenzi wake wa miaka sita mwendo wa saa saba mchana.
Mpenzi huyo alitaka amtembelee. Akiwa na furaha kwamba angetumia Siku ya Wapendanao na mpenzi wa maisha yake, aliaga familia yake kwa haraka.
Ng’endo hakujua kuwa huo ulikuwa mtego na siku ya Valentino.
Bila wasiwasi wowote, alijiandaa na kuanza safari ya kuelekea jijini mwendo wa saa kumi jioni, akiwa na hamu ya kukutana na kipenzi cha moyo wake lakini hakujua kuwa mtego wa kifo ulikuwa mbele yake.
Alipofika, alimpigia simu dadake mdogo, Caroline Wandia, na kumthibitishia kwamba alikuwa amefika salama jijini na alikuwa na mpenzi wake wakielekea Kajiado.
Mnamo Februari 3 familia ilimpigia simu Ng’endo. Walishtuka kupata simu ilikuwa imezimwa. Familia ilishuku kulikuwa na kitu kibaya lakini waliamua kusubiri kidogo kuona ikiwa binti yao angefungua simu.
Lakini mnamo Februari, 4 mpenzi huyo alipigia simu familia na kutania kwamba yeye na Ng’endo walikuwa wamesafiri kwa ndege hadi Amerika na wangekaa huko kwa miezi kumi.
“Mpenzi huyo alizungumza nami kupitia simu yangu, akisema yeye na dada yangu walikuwa wamesafiri hadi Amerika lakini nilitilia shaka. Nilimuuliza mpenzi wa dada yangu ikiwa inawezekana kusafiri hadi Amerika bila pasipoti. Alijibu kuwa yeye ni afisa wa serikali na hawahitaji pasipoti za kusafiri hadi Amerika,” alisema Bi Wandia.
Mnamo Februari 5, familia ilipata mshtuko ilipopokea habari kuwa mwili wa Ng’endo uliokuwa ukioza ulipatikana katika nyumba moja eneo la Kajiado ambapo mpenzi wake alikuwa ameajiriwa kufanya kazi shambani.
“Tulipokea habari kutoka kwa polisi wa Kajiado kwamba mwili wa binti yetu ulipatikana ndani ya nyumba na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti jijini Nairobi,” alisema Bi Wandia kwa kufichua kuwa familia ilitambua mwili kuthibitisha kuwa ni wa binti yao.
“Meno ya binti yangu yalikuwa yameng’olewa huku uso wake ukiwa umeharibika kabisa,” alisema Bw James Munene 52, babake marehemu.
Uchunguzi wa maiti ulibaini kuwa Ng’endo alifariki kutokana na majeraha aliyopata kichwani.
“Sikuamini binti yangu alikuwa amekufa hadi nilipomuona akiwa amejeruhiwa vibaya na mwili wake katika chumba cha maiti,” alisema Bw Munene.
Munene alisimulia jinsi mpenzi huyo alivyokuwa akimtembelea bintiye mara nyingi nyumbani na hakuwahi kuonyesha dalili za tabia mbaya.
“Mshukiwa angemtembelea binti yangu hapa Kirinyaga na kurudi Kajiado alikofanya kazi. Wakati huu wote alijifanya afisa wa usalama lakini baadaye tukapata habari kwamba alikuwa ameajiriwa shambani huko Kajiado,” alisema Bw Munene.
Bw Munene alisema mshukiwa huyo anatoka Kericho na bintiye aliyeuawa alikuwa akienda huko kumsalimia.
“Binti yangu na mshukiwa walikuwa marafiki wakubwa. Walikutana Nairobi 2019 na wakapendana. Binti yangu alikuwa akifanya kazi ya nyumbani Nairobi alipokutana na mshukiwa na tangu wakati huo walikuwa wakihusiana sana,” alisema Bw Munene.
Baada ya hapo Ng’endo alirudi nyumbani na kuanzisha duka na kabla ya kifo chake biashara yake ilikuwa ikiendelea vizuri.
Haikuweza kufahamika mara moja kwa nini mshukiwa alikatiza maisha ya Ng’endo ambaye familia ilimtaja kuwa mtu mchapakazi.
“Binti yetu alichukulia kazi yake ya biashara kwa uzito. Tulimpenda sana lakini cha kusikitisha ni kwamba aliuawa na mtu wa karibu sana kwake. Kifo cha binti yetu kitasalia katika akili zetu milele,” alisema Bw Munene.
Familia hiyo sasa inalilia haki baada ya mpenzi wa binti yao aliyeuawa kwenda mafichoni.
“Maafisa wa usalama wa Kajiado walitufahamisha kuwa ni mshukiwa aliyewapigia simu na kuripoti kwamba alikuwa amemkatakata binti yetu hadi kufa. Baada ya kuwaarifu polisi, mshukiwa alitorokea kusikojulikana,” alisema Bw Munene.
Familia hiyo inaitaka Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) kuchunguza kwa kina mauaji hayo.
“Tunataka kujua ni kwa nini mshukiwa alimuua binti yangu. Pia tunataka mshukiwa asakwa na kufunguliwa mashtaka. Tunachotaka ni haki itendeke,” aliongeza Bw Munene.
Marehemu atazikwa Ijumaa Februari 14 nyumbani kwa wazazi wake Kirinyaga ya Kati.