Joto walilofurahia wabunge wa Azimio katika ‘viti vya serikali’ lilivyozimwa ghafla
BAADA ya kufurahia ‘joto’ kwenye viti vya upande wa walio wengi kwa siku mbili, wabunge wa Azimio Jumatano, walikubali kubanduka kutoka viti hivyo baada ya Spika Moses Wetang’ula kuamua kuwa Kenya Kwanza ndio mrengo wa walio wengi.
Wakiongozwa na Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo wabunge hao, hata hivyo, walisema japo walikubali uamuzi kutii uamuzi wa Wetang’ula hawakubaliani nao.
“Kama Azimio tunatii uamuzi wako kulingana na hitaji la sheria za kudumu nambari 187 (2) na sitaibua suala lolote tena. Lakini kwa heshima kuu, tunakataa uamuzi huu kwa sababu ‘umekanyaga miguu yetu’,” akaeleza Bi Odhiambo, ambaye ni kiranja wa walio wachache.
“Kama Azimio tutachukua hatua nyingine,” akaongeza bila kufichua hatua yenyewe.
Awali, Bw Wetang’ula alikuwa ametangaza kuwa Kenya Kwanza ndio mrengo wa walio wengi na Azimio ndio mrengo wa walio wachache.
“Kwa mujibu wa idadi ya wabunge waliochaguliwa kwa tiketi za vyama tanzu katika kila muungano, Kenya Kwanza ina jumla ya wabunge 165 huku Azimio ikiwa na wabunge 154 katika bunge hili. Kwa hivyo, Kenya Kwanza ndio walio wengi na Azimio ni walio wachache,” akasema kwenye taarifa aliyosoma alasiri.
Bw Wetang’ula alitoa uamuzi huo siku moja baada ya wabunge kujadili uamuzi wa Mahakama Kuu uliobatilisha uamuzi wa Bw Wetang’ula wa Oktoba 6, 2022 kwamba Kenya Kwanza ndio mrengo wa walio wengi.
Katika uamuzi wao wa Ijumaa Februari 7, 2025, majaji Jairus Ngaa, John Chigiti na Lawrence Mugambi walisema kuwa uamuzi wa Wetang’ula ni batili kwani unakiuka kipengele cha 108 cha Katiba.
Kufuatia uamuzi huo wabunge wa Azimio, Jumanne, walikalia viti vilivyo upande wa kulia wa Spika ambavyo kawaida hukaliwa na wabunge wa mrengo wa walio Serikalini.
Kulingana na wabunge hao, wakiongozwa na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, uamuzi wa mahakama uliashiria kuwa mrengo wao ndio wa walio wengine.
“Ni fahari yangu kukalia kiti cha Kiongozi wa Wengi. Nimegundua kuwa kiti hicho kina joto……. Sidhani kama nitabanduka kutoka kiti hiki,” Bw Mohamed akaeleza huku wabunge wengine wakiangua kicheko.