Jamvi La Siasa

Hatutamruka Ruto na haturejei kwa maandamano, washirika wa Raila wasema

Na CECIL ODONGO February 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amewaongoza wanasiasa wa chama hicho kushikilia kuwa ataendelea kuunga mkono Rais William Ruto hata baada ya kupoteza uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) wikendi.

Bw Odinga Jumamosi alibwagwa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf kwenye kinyanga’nyiro cha AUC baada ya kuendesha kampeni kali Afrika.

Wengi hasa kutoka ukanda wa Mlima Kenya na baadhi ya vijana Jumamosi walishabikia kushindwa kwa Raila huku wakimrai arudi nchini na kuendeleza shinikizo na maasi dhidi ya Rais Ruto kama zamani.

Hata hivyo, Bw Odinga Jumapili alimiminia Rais Ruto sifa kedekede akimwondolea lawama na kumwonya yeyote ambaye atamhusisha na kutofaulu kwake AUC.

“Kuna wale ambao watasema kuwa Rais Ruto alitaka tu kuhangaisha baba lakini hawaelewi kuwa mimi ndiyo nilitangaza kuwa nawania wadhifa huu binafsi. Rais Ruto alikuja tu na kusema ataniunga mkono,” akasema Bw Odinga.

 Alikuwa akizungumza wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na ubalozi wa Kenya jijini Addis Ababa kwa heshima yake na Wakenya walioandamana naye.

“Ningependa kusema kuwa Rais Ruto alifanya kila kitu kunisaidia na siwezi kulalamika hata kidogo. Alinipa msaada wote wa kuzuru Afrika na kuweka miadi ili nikutane na viongozi wote na ikafanyika hivyo. Hatufai kujuta wala sijutii kuwa nilishiriki kinyángányiro hiki,” akaongeza.

Waziri huyo mkuu wa zamani alisema kuna masuala mengine ambayo yalisababisha kushindwa kwake na baada ya kipindi kifupi kitajulikana na umma.

Waziri huyo mkuu aliwakumbusha waliokwepo kuhusu kauli aliyosema Jumatatu wiki jana kuwa alikuwa tayari kwa matokeo yoyote kwenye uwanizi wa AUC.

“Nilisema tukishinda, tumeshinda na tukipoteza, bado tumeshinda. Kwa hivyo, tulipoteza na tumeshinda wala sijutii jambo lolote,” akasema Bw Odinga.

Kauli ya Raila sasa inazima kinywa cha waliokuwa wakiomba ashindwe ili kumpiga vita Rais Ruto, wengine wakilaumu kiongozi wa nchi kwa kusababisha kubwagwa kwake.

Kumekuwa na madai ya baadhi ya Wakenya kuwa kiongozi huyo alitumia maandamano ya Gen Z mnamo Juni mwaka jana ili kuingia kwenye serikali jumuishi na Rais Ruto.

Mitandaoni, baadhi ya Wakenya, walifasiri kulemewa kwa ‘Baba’ kama ishara ya uhusiano mbaya wa kidiplomasia ambao utawala wa Kenya Kwanza, unao na mataifa mengine Afrika.

Walitaka waziri huyo mkuu arejee nchini na kuwasaidia kupambana na utawala huu waliolalamika kuwa umeongeza ushuru na kuanzisha miradi ambayo haizingatii maslahi ya raia.

Wandani wa Bw Odinga, wakiongozwa na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed jana walisema kuwa licha ya matokeo ya AUC, bado hawatabanduka katika kuunga utawala wa Rais Ruto.

“Ningependa kumshukuru Rais Ruto kutokana na msaada wake kwa Raila katika uchaguzi huu wa AUC na tunawaomba Wakenya wote wajiandae kumkaribisha Raila kishujaa atakaporejea nyumbani,” akasema Bw Mohamed ambaye aliwaongoza viongozi wa ODM kuonyesha uaminifu wao kwa serikali jana.

“Uchaguzi huu haukuwa kwa sababu ya ushindi wa mtu binafsi bali taifa na Afrika nzima. Kwa hivyo, sisi sote ni washindi wala hakuna haja ya kumlaumu yoyote,” akasema Bw Mohamed.

Mbunge wa Makadara George Aladwa naye alisema wanaodhani Raila sasa atarudi kumpiga vita Ruto wanaota wala hawawezi kusambaratisha serikali ambayo wanaihudumia.

“Sisi tuko kwa serikali na wale ambao wanasherekea kushindwa kwa Raila ndiyo arudi aanze vita na Ruto, hawajui kile wanachosema. Kuna baadhi ya watu ambao wanafikiria tutarudi kushirikiana nao ilhali wametusaliti hapo awali. Sisi haturudi kwenye maandamano,” akasema Bw Aladwa.

“Sote tutaunga mkono Rais Ruto kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kujitolea kuunga azma ya Baba. Sisi si watu wa kulipa mazuri kwa mabaya na kile Raila amesema ndiyo tunafuata, walioko upinzani, wapambane na hali yao,” akaongeza mwenyekiti huyo wa ODM, Kaunti ya Nairobi.

Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Martin Andati naye anasema hoja kuu itakuwa Raila kumsaidia Rais kumaliza matatizo yanayowasibu Wakenya.

“Siasa hubadilika lakini wakishirikiana kumaliza changamoto za Wakenya basi ushirikiano wao utafaulu,” akasema Bw Andati.