Seneta Cheptumo aliyembwaga Gideon Moi uchaguzini aliugua kwa muda akilazwa hospitalini
RAIS William Ruto Jumapili aliwaongoza Wakenya kuomboleza mauti ya Seneta wa Baringo William Cheptumo.
Marehemu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 57 katika hospitali moja jijini Nairobi na amekuwa akiugua maradhi ambayo hayakufichuliwa.
“Seneta William Cheptumo alikuwa kiongozi shupavu ambaye alitumikia vyema umma. Alikuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wakazi wa Baringo,” akaandika Rais William Ruto kwenye rambirambi yake.
“Maombi yetu ni kwa familia, marafiki na wakazi wa Baringo. Lala salama mheshimiwa,” akaongeza.
Spika wa Seneti Amason Kingi alisema kuwa marehemu alichukua majukumu yake kwa uzito na mara kwa mara alikuwa akitetea maslahi ya wakazi wa Baringo.
“Kenya imepoteza kiongozi ambaye alikuwa na imani katika ugatuzi. Naungana na familia yake, watu wa Baringo na Wakenya wote katika kumwomboleza,” akasema Bw Kingi.
Kwa mujibu wa wabunge Kiborek Reuben (Mogotio) na Jackson Kosgei (mteule), seneta huyo amekuwa akiugua na aliruhusiwa kupumzika nyumbani baada ya kuondoka hospitalini mnamo Februari 9.
Baada ya kuhudumu kama Mbunge wa Baringo Kaskazini kwa mihula mitatu, Bw Cheptumo ambaye anatoka milima ya Bartabwa, alimbwaga Gideon Moi katika kura ya 2022.
Alimpiku Bw Gideon, mwanawe rais wa pili marehemu Daniel Moi kwa kuzoa kura 141,777 dhidi ya Bw Gideon ambaye alipata kura 71,408.
Ushindi huo ulitamatisha ubabe wa familia ya Moi katika siasa za kaunti hiyo.
Kando na siasa, Bw Cheptumo alifahamika sana kwa kupendekeza suluhu kwa ukosefu wa amani katika kaunti hiyo na Kaskazini mwa Bonde la Ufa. Eneo hilo limekuwa likishuhudia visa vya ujangili pamoja na wizi wa mifugo.
Kwenye Bunge la Seneti alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama, Ulinzi na Masuala ya Kigeni. Katika Bunge la Kitaifa kati ya 2008-2022 alihudumu kwenye kamati mbalimbali na alikuwa mwenyekiti wa kamati ya sheria na haki.
Kati ya 2008-2013, alihudumu kama waziri msaidizi wa Haki na Masuala ya Katiba. Maseneta Otieno Kajwang’ (Homa Bay) na Karungó Thang’wah (Kiambu) ni kati ya walioomboleza mauti yake.