Habari

Mbunge wa Malava Moses Malulu Injendi afariki akitibiwa hospitalini

Na FATUMA BARIKI, CHARLES WASONGA February 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Malava, Bw Moses Malulu Injendi ameaga dunia, Spika wa Bunge Moses Wetang’ula.

Spika Wetang’ula alitoa tangazo hilo Jumatatu akisema mbunge huyo wa muhula wa tatu alifariki Februari 17, 2025 saa kumi na moja jioni akipokea matibabu katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

“Waheshimiwa Wabunge, ni kwa huzuni kwamba ninawaarifu kuhusu kifo cha mwenzetu Mheshimiwa Moses Malulu Injendi ambaye alituacha leo jioni Februari 17, 2024 saa kumi na moja na nusu jioni katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi,” akasema.

Bw Injendi, ambaye alikuwa akihudumu muhula wake wa tatu bungeni, alikuwa Naibu Mwenyekiti was Kamati ya Bunge kuhusu Elimu.

Bw Wetang’ula alimtaja Bw Injendi kama mbunge aliyewakilisha watu wa eneo bunge lake kwa moyo wa kujitolea na uadilifu wa hali ya juu.

“Michango yake katika michakato ya utungaji sheria haswa sekta ya Elimu na kilimo cha miwa, na uliolenga kuimarisha maisha ya Wakenya, itakoswa,” akaeleza.

Bw Injendi alichaguliwa kwa mara ya kwanza Bungeni katika uchaguzi mkuu wa 2013 kwa tiketi ya chama cha Amani National Congress (ANC).

Alirejea bunge baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 kwa tiketi ya chama cha ODM.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Injendi alistahimili mawimbi ya chama cha ODM na muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya na kuhifadhi kiti chake kwa tiketi ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).