Wagonjwa kuteseka zaidi hospitali za kibinafsi zikikataa SHA
ZAIDI ya hospitali 600 ambazo ni sehemu ya Muungano wa Hospitali za Kibinafsi za Vijijini na Mijini nchini Kenya (RUPHA), zimetangaza kuwa kuanzia Jumatatu 24 zitasitisha huduma zote chini ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) katika vituo vyao.
Dk Brian Lishenga, mwenyekiti wa muungano huo aliwaambia waandishi wa habari Jumatano asubuhi kwamba wameafikia uamuzi huo kwa sababu ya kutolipwa na serikali, na mfumo ambao unatatizika wa kulipia wagonjwa wanaotibiwa na kurudi nyumbani chini ya SHA.
“Kama wataalamu wa afya, jukumu letu la kwanza ni ustawi wa wagonjwa wetu. Hata hivyo, kuendelea kushindwa kutatua changamoto kubwa katika kipindi cha mpito cha SHA, sasa kunahatarisha moja kwa moja ubora na uendelevu wa huduma katika hospitali zetu,” alisema Dkt Lishenga.
“Uamuzi huu haujafanywa kirahisi. Unafuatia miezi kadhaa ya mazungumzo ambayo hajafanikiwa, ahadi ambazo hazijatekelezwa, na kuongezeka kwa shida za kifedha miongoni mwa hospitali, ambazo sasa zinatishia taasisi za afya kote nchini Kenya,” aliongeza.
Wanachama hao kupitia viongozi wao walisema wameshindwa kufikia muafaka na serikali katika masuala mawili muhimu: malimbikizi ya takriban Sh30 bilioni kutoka kwa iliyokuwa Hazina ya Kitaifa wa Bima ya Afya (NHIF) na mfumo unaosumbua wa kulipia wagonjwa wa kutibiwa na kurudi nyumbani chini ya SHA.
Dkt Lishenga anasema kwamba madeni wanayodai NHIF ambayo iliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Hazina ya Afya Jamii chini ya SHA ni ya kuanzia 2017.
“Madhara yake yamekuwa mabaya sana, yamesababisha watu kupoteza kazi, kusumbuliwa na benki, uhaba wa dawa muhimu, madaktari wasiolipwa pamoja na mzigo wa kodi kwa mapato ambayo hayapo,” alisema Dkt Lishenga.
Dkt Lishenga alisema ni jambo lisilowezekana kwa serikali kulipa Sh75 pekee kwa kila mgonjwa ndani ya mwezi mmoja.
“Mtindo huu ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wa wagonjwa, na kulazimisha hospitali kuchukua hatua za kupunguza gharama ambazo zitaathiri ubora wa huduma za afya. Tunakataa kuweka maisha ya Wakenya hatarini,” akasema.
Uamuzi wao unajiri siku chache baada ya naibu wa rais Prof Kithure Kindiki kukiri kwamba serikali inafaa kusikiliza washikadau wote ili kurekebisha SHA miezi mitano baada ya kuanza kutumika.
Prof Kindiki alisema kuwa maafisa wa wizara ya Afya wana hadi mwisho wa mwezi huu kutafuta suluhu kwa matatizo yote ya SHA kabla ya kuanzisha kampeni ya usajili nchini kote.
Dkt Lishenga pia alisisitiza kuwa hawajaondoa kauli yao ya awali ya kusitisha huduma kwa walimu na maafisa wa polisi chini ya kampuni ya Medical Administrator Kenya Limited (MAKL).
“MAKL imeshindwa kulipa hospitali kwa zaidi ya miezi 11. Pia inapendelea hospitali zake kwa njia isiyo na ushindani na isiyozingatia maadili,” alisema Dkt Lishenga.
“Iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kupata suluhu, walimu na maafisa wa polisi wataachwa bila huduma bora za afya,” aliongeza.