Makala

Wanamazingira wataka suluhu uchafuzi wa Ziwa Victoria ukizidi

Na GEORGE ODIWUOR February 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAMAZINGIRA wameelezea wasiwasi kuhusu uchafuzi wa Ziwa Victoria kupitia utupaji wa plastiki zinazotishia viumbe wa majini na mamilioni ya watu wanaolitegemea.

Ziwa hilo linakabiliwa na changamoto kubwa likiendelea kuchafuliwa kwa taka za plastiki kutoka kwa wavuvi na vyanzo vingine.Baadhi ya plastiki husombwa hadi ziwani mvua inaponyesha.

Kwa upande mwingine, wavuvi hutupa taka kama vile mifuko ya plastiki moja kwa moja ndani ya ziwa na kuathiri mfumo ikolojia na idadi ya samaki wanaolitegemea kwa riziki zao.

Wakati wa kuvua samaki, nyavu zinahitaji kuwa na sehemu za kuelea ambazo zinawekwa juu ya maji na nanga zinazozishikilia chini karibu na kingo za ziwa.

Lakini katika jitihada za kupunguza gharama, wavuvi katika Ziwa Victoria wanatumia vifaa vilivyoboreshwa na visivyo vya kawaida kutengeneza sehemu za kuelea na kutia nanga.Vifaa vinavyotumiwa kuweka nyavujuu ya maji ni pamoja na mbao au plastiki.

Hata hivyo, wavuvi hao hutumia chupa za maji za plastiki.Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufuo wa Suba Kusini, Bw William Onditi, alisema wavuvi wanapendelea kutumia chupa za maji za plastiki kwa sababu ni nafuu.

“Mtu anaweza kuokota chupa za maji kwa urahisi kutoka jaani na kuzitumia,” anasema.

Anabainisha kuwa vifaa mahususi kwa uvuvi vinagharimu takriban Sh50,000.“Hakuna mvuvi aliye tayari kutumia kiasi hicho ikiwa anachopata kutoka ziwani ni sehemu ndogo tu ya kiasi hicho. Kwa hivyo wanatafuta njia nafuu, ‘anasema.

“Ni kweli chupa hizo zinachafua ziwa. Lakini hakuna chochote ambacho wavuvi wanaweza kufanya kwa sababu ya changamoto za kiuchumi zinazokumba sekta hii,” Bw Onditi asema.

Hata hivyo, wanamazingira wana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya plastiki katika ziwa hilo, jambo ambalo wanasema huenda likaleta madhara ya muda mrefu kwa viumbe wa baharini na binadamu.

Bw Willis Omullo, mtetezi wa mabadiliko ya hali ya hewa katika Aluora Makare, shirika la jamii la kuhifadhi mazingira huko Homa Bay, anasema sio tu nyenzo zinazoelea ambazo huchafua ziwa, lakini zana zingine za uvuvi pia.Anasema nyenzo nyingi zinazotumika kuvua samaki ni za plastiki na baadhi ni hatari kwa mazingira zinapotupwa vibaya.

Bw Omullo anasema ana wasiwasi kuhusu hali ya plastiki ambazo haziozi, ambazo zinadhuru viumbe vya baharini.