Wabunge wafichua Sh73 bilioni zilizofichwa katika bajeti ya Ruto
KAMATI ya Bunge imefichua takwimu zinazokinzana zinazoonyesha tofauti ya Sh73 bilioni katika stakabadhi za bajeti zilizowasilishwa na Hazina ya Kitaifa katika makadirio ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026.
Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipango ya Kitaifa imetaka majibu kuhusu takwimu gani kati ya mbili zilizowasilishwa ni sahihi kwa matumizi ya serikali katika mwaka mpya wa fedha.
Stakabadhi zilizowasilishwa na Hazina ya Kitaifa zinaonyesha Sh4.263 trilioni kama kiasi cha bajeti kwa mwaka wa kifedha wa 2025/26 lakini pia inataja Sh4.336 trilioni kama matumizi ya jumla, na kutia shaka kuhusu tofauti ya Sh73 bilioni.
Hazina ya Kitaifa ilikuwa imefika mbele ya kamati kufafanua Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026.
Mwenyekiti wa kamati Kimani Kuria alifichua hali hiyo isiyo ya kawaida na alipowashinikiza maafisa wa Hazina, hakuweza kupata jibu la haraka kuhusu suala hilo.
“Nimebaini kuwa kuna tofauti katika Taarifa ya Sera ya Bajeti kutoka Hazina. Ipi ni ipi?” Bw Kuria aliuliza kuhusu takwimu zinazokinzana.
Hata hivyo, maafisa wakuu wa Hazina wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Huduma za Uhasibu Benard Ndung’u hawakuweza kutoa jibu la haraka. Badala yake, waliomba kuwasilisha baadaye hati iliyo sawa.
“Bw Mwenyekiti tutawasilisha hati yenye takwimu sahihi,” Bw Ndung’u alijibu.
Bw Kuria alisema hakuna njia hati ya bajeti inaweza kuwa na takwimu mbili tofauti.
“Huwezi kuwa na takwimu tofauti kwa bajeti moja. Haiwezi kutokea tu,” Bw Kuria alisema.
“Sh73 bilioni ni kiasi ambacho hatupaswi kupuuza tu. Tunahitaji takwimu moja,” Bw Kimani aliongeza.
Kufikia wakati ambao wabunge hao waligundua tofauti hizo, Katibu wa Hazina Chris Kiptoo ambaye alikuwa amefika kwa muda katika kamati hiyo alikuwa tayari ameondoka. Katibu alifahamisha wabunge kuwa amefiwa na alihitajika katika mochari ya Lee Funeral.
Aliacha timu ya maafisa wakuu wa hazina ambao alisema wana uwezo wa kujibu maswali yote kutoka kwa wabunge.