Habari za Kitaifa

Aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ameaga dunia

Na LUCY KILALO, LABAAN SHABAAN February 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ameaga dunia.

Bw Chebukati amefariki katika Nairobi Hospital baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Msemaji wa familia yake, Bw Eric Nyongesa athibitisha kifo hicho akieleza kuwa Bw Chebukati alifariki muda mfupi kabla ya saa tano usiku Alhamisi, Februari 20, 2025.

Familia hiyo ambayo Ijumaa Februari 21, 2025 ilikongamana katika makafani ya Lee, Nairobi,  imeomba faragha inapomuomboleza marehemu.

Rais William Ruto ametuma rambirambi zake kwa familia ya Bw Chebukati akielezea kupokea habari za kifo chake kwa huzuni kubwa.

“Nimepokea habari za kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kwa huzuni kubwa. Alikuwa kiongozi mwenye msimamo na mwadilifu ambaye alitumikia nchi yetu kwa uadilifu. Kifo chake ni pigo kuu kwa nchi yetu. Fikra na maombi yetu yako na familia yake na marafiki katika wakati huu mgumu. Pumzika kwa amani,” Rais amesema kwenye rambirambi zake.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula pia amewasilisha rambirambi zake akitaja kifo chake kuwa pigo si kwa taifa tu bali kwa jamii ya wanasheria.