Anavyotumia Azolla kupunguza gharama ya ufugaji
GEORGE Muturi ambaye ni mkulima eneo la Limuru, Kaunti ya Kiambu, amekuwa mfugaji kwa zaidi ya miaka 10.
Kilimo, ni kazi aliyoingilia baada ya kukamilisha masomo ya Shule ya Upili.
Alianza na kuku, akiwa mwingi wa matumaini kwamba mkondo aliochukua ungemfaa siku za usoni.
“Nilianza na kuku wa kienyeji, hususan kwa minajili ya biashara ya mayai,” Muturi anasema.
Hata hivyo, gharama ya juu ya malisho nusra izime ndoto zake.
Wafugaji wanalalamikia gharama ya juu ya chakula, hasa cha kuku – malighafi yakichochea mfumko wa bei.\

Ni kupitia utafiti aliofanya kwenye intaneti, ambapo Muturi aligundua njia mbadala kupunguza gharama.
Kando na matumizi ya wadudu wekundu (red earth worms) na Black Soldier Fly (BSF), kijana huyu amekumbatia matumizi ya Azolla kupunguza gharama.
Azolla ni mmea wa majini uliosheheni virutubisho vya Nitrojini hivyo basi kuwa bora kama kiungo cha mbolea asilia (biofertiliser).
Mmea huo, vilevile unatumika kama malisho ya mifugo.
Kwa sasa, Muturi ana kuku wapatao 200, samaki akikadiria kuwa 2, 000 na sungura 70.
“Hutumia Azolla kulisha kuku, kwa kuwa ni chakula bora chenye virutubisho vya Protini ya mimea,” anasema.
Francis Faluma, mtaalamu wa masuala ya kilimo anasema Azolla ina kati ya asilimia 20 hadi 30 ya virutubisho vya Protini.

“Ni muhimu mfugaji yeyote yule awe na njia za kushusha gharama endapo anataka kuunda faida na kusalia kwenye biashara. Kwa wafugaji wa kuku, Azolla na BSF ndio suluhu,” anasema mtaalamu Faluma kutoka Serikali ya Kaunti ya Kakamega.
Kupitia mbinu mbadala anazotumia, anakadiria kupunguza gharama ya malisho kwa karibu asilimia 30.
Azolla huelea juu ya maji, na aghalabu wakulima huipanda kwenye vidimbwi.
“Mmea huu hauna kazi nyingi kuukuza,” Muturi anakiri, akihimiza wakulima wenye mashamba madogo na wanaoendeleza ufugaji kuukumbatia.
Aidha, unahitaji maji yenye kiwango cha asidi cha kati ya pH 5.5 na 7.5.
Mbegu zake, ni Azolla zilizovunwa na kurejeshwa dimbwini.

Mmea huu huchukua kati ya siku 10 hadi 15 pekee kukomaa baada ya upanzi.
Unaboreshwa kwa kutumia mbolea ya mifugo, ya kuku ikiwa bora zaidi.
Jinsi ya kuvuna, ni kuuokota kwa kichujio.
Wakulima wanahimzwa kuweka chandarua juu ya dimbwi, ili kuokoa Azolla dhidi ya kushambuliwa na ndege.