Kadi nne za Raila kuelekea 2027
WANANCHI wanasubiri kuona karata za kisiasa ambazo Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga atazicheza baada ya kubwagwa alipowania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Kulingana na wachambuzi wa kisiasa, Bw Odinga anatazamiwa kufuata njia nne anaposawiri upya mustakabali wake wa kisiasa nchini.
Moja ya mikakati ni kuimarisha uhusiano na Rais William Ruto akilenga kumega nafasi zaidi katika serikali ya Kenya Kwanza.
Mchanganuzi wa Kisiasa Peter Kagwanja anatabiri Bw Odinga ataendelea kuhusika zaidi katika serikali.
“Ninadhani kuwa kuanzia sasa na Januari ama Machi mwaka ujao, ataendelea kutikisa mashua ya Kenya Kwanza ili washirika wake wapate nyadhifa serikalini,” akasema Prof Kagwanja.
Alirejelea kuwa Bw Odinga alitoa kidokezo cha kuimarisha ushirikiano na Rais Ruto.
Kiongozi huyu wa upinzani wa miaka mingi pia anatarajiwa kuweka serikali katika mizani na kuikosoa huku akijiandaa kuwania urais kwa mara ya sita ufikapo 2027.
“Atakaporejea nchini, huenda Bw Odinga akaandaliwa hafla ya umma katika moja ya ngome zake ambazo Dkt Ruto alikuwa anajaribu kurithi. Bw Odinga ataunganisha ngome zake ili azitumie kutafuta mamlaka zaidi na rasilimali za kisiasa,” akasema Prof Kagwanja akiongeza kuwa Dkt Ruto anaweza kudinda kukubali matakwa ya Bw Odinga.
“Bw Odinga hajawahi kukosolewa katika kiwango ambacho anakashifiwa kwa kuwasaliti watu. Kufikia Juni/Agosti mwaka mmoja kabla ya uchaguzi, ataanza kujipanga awe rais ama mwanasiasa mwenye ushawishi ambaye atafaulu kupigia debe mwaniaji atakayeibuka kuwa rais,” Prof Kagwanja akabashiri.
“Ni wazi anaeleweka vyema akiwa mfalme badala ya anayemfanya mtu kuwa mfalme.”
Kulingana na mchambuzi huyu wa siasa, kufikia Machi au Mei 2027, kabla ya uteuzi, anaamini aliyekuwa waziri mkuu atakuwa ameamua anachotaka.
Yamkini njia nyingine ambayo Bw Odinga anaweza kufuata ni kuungana tena na viongozi wenzake wa mrengo wa upinzani kama vile Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Bw Kalonzo amenukuliwa awali akishauri bosi wake wa zamani asiingie katika serikali ya Kenya Kwanza ili aaminike tena na Wakenya kama awali.
“Anafaa kuhuisha sifa zake kuwa mtu ambaye alipigania demokrasia. Anawezaje kupoteza sifa hizi zote kwa kushirikiana na madikteta katika serikali ya Kenya Kwanza? Iwapo ODM itaamua kujiunga na Ruto watashindwa,” Bw Kalonzo alisema mnamo Februari 22, 2025 akiwa Kaunti ya Kirinyaga.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amemkanya kiongozi wake dhidi ya kumuunga mkono Rais Ruto.
“Iwapo ataamua kumuunga mkono Rais, nitampa ushauri wenye uwazi kuwa utakuwa uamuzi mbaya,” akasema Bw Sifuna alipohojiwa katika runinga moja nchini.
Chaguo jingine la Bw Odinga, kulingana na wanasiasa na wachambuzi, ni kushirikiana na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kumng’oa Rais Ruto madarakani 2027.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Bw Gachagua ndiye mwanasiasa mwenye nguvu zaidi anayeweza kumbandua Dkt Ruto.
Mchanganuzi wa kisiasa Gasper Odhiambo anasema kuwa Rais Ruto anatumai Bw Odinga hataungana na vijana wa kizazi cha Gen Z ambao tayari wamepigiwa debe na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta hadharani.
Bw Odhiambo pia anadhani Dkt Ruto hatazamii kuwa Bw Odinga atafuata mkondo wa kuanzisha maandamano dhidi ya serikali.
“Lazima Ruto alikuwa na matumaini ya kuwa Bw Odinga angeshinda uchaguzi wa AUC ili arithi ngome zake za kisiasa akiwania urais tena 2027,” akasema Bw Odhiambo.