Mji wa nyumbani kwa Rais Moi wakosa stima mwaka mzima sababu ya bili kubwa
SEHEMU nyingi katika mji wa Kabarnet, ambao ni makao makuu ya Kaunti ya Baringo, zimesalia gizani kwa muda wa mwaka mmoja baada ya umeme kukatizwa kutokana na deni kubwa la bili ya umeme.
Mji huo ukikosa taa za barabarani, serikali ya kaunti nayo imekuwa ikidai haina fedha za kulipia deni hilo huku wakazi na wakikosa kuridhika na msimamo huo.
Ukosefu umesababisha uhalifu kuongezeka huku visa vya wizi wa kimabavu pia vikiongezeka. Watu kadhaa wameuawa na wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.
Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Kasoiyo, Kapkut, Barabara ya Hospitali, Barabara ya Valley, Kaptimbor, Uwanja wa maonyesho, Police Line, na Cereals, ambapo wahalifu wanawaandama wanaotembea.
Mfanyabiashara Noel Yegon alisema wezi hao wamekuwa wakilenga maduka ambayo yapo katika maeneo yaliyogizani.
“Kumekuwa na visa vingi vya maduka kuvunjwa. Wafanyabiashara katika soko la Kabarnet pia, wanalalamika wezi wanapora bidhaa zao usiku, hasa vyakula. Itakuwa busara kwa wahusika kuhakikisha taa za barabarani zinarejeshwa ndani ya manispaa. Hali hii inalemaza biashara,” alisema Bw Yegon.
Mwanaharakati wa haki za binadamu, Isaiah Biwott, alilaani hali hiyo, akiitaja kuwa aibu kwa wafanyabiashara kulipia kodi bila kupata huduma zinazofaa.
Mwakilishi wa Wadi ya Kabarnet Ernest Kibet, alisikitishwa na hali kuwa taa za barabarani hazijarejeshwa kwa muda wa mwaka mmoja.
“Hatufurahishwi kwa kukatizwa kwa umeme katika mji huu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Haja gani kuwa na bodi ya manispaa ikiwa huduma ambazo zinapaswa kufanyika kila siku hazipatikani?,”
Watu hawawezi kufanya biashara gizani. Serikali hii inachangia kutokuwa na usalama katika mji huu,” akaongeza Bw Kibet.
Alieleza kuwa mji huo ni kitovu cha biashara na hapo awali, watu waliendesha biashara kwa saa 24, lakini sasa wanalazimika kufunga mapema.
Afisa wa Kaunti ya Baringo anayehusika na makazi na mipango ya miji, Bw Reuben Ruto, alilaumu hali hiyo kwa ucheleweshaji wa mgao wa fedha kutoka Hazina ya Kifedha.
Alieleza ucheleweshaji huo, umechangia kaunti kushindwa kulipa bili za umeme, ambazo zimefikia karibu milioni moja.
“Tumelipa sehemu ya deni na taa zimewashwa katika baadhi ya barabara. Mifumo ya taa za jua inahitaji matengenezo na kubadilishwa, lakini bado hatuna bajeti kwa sasa kutokana na uhaba wa rasilimali katika kaunti,”
“Hata hivyo, tunashughulikia suala hili na tunatarajia kulitatua ndani ya miezi miwili,” alisema Bw Ruto.