Habari

Ruto: Niliandikia Askofu Lai ujumbe kwamba naja kanisani ila alikawia kujibu

Na BRIAN OCHARO February 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto ameeleza sababu ya kuchelewa kuhudhuria ibada kuu ya Jumapili katika kanisa la Askofu Wilfred Lai la Jesus Celebration Centre (JCC) mjini Mombasa.

Kwa mujibu wa Rais Ruto, alichelewa kutokana na ujumbe Askofu huyo aliokawia kujibu ujumbe mfupi wa WhatsApp aliomtumia usiku wa Jumamosi, na pamoja na majukumu ya asubuhi katika bandari ya Mombasa.

“Usiku wa Jumamosi kabla ya kulala, nilimtumia Askofu Lai ujumbe wa WhatsApp nikimfahamisha kuhusu nia yangu ya kuhudhuria ibada ya Jumapili asubuhi. Nilikuwa nimepanga kuhudhuria hafla ya utalii asubuhi hiyo, lakini nikasema sitaenda, bali nitaipa kanisa kipaumbele,” alieleza.

“Nilihisi moyoni mwangu hitaji la kuja kumsikiliza mtumishi huyu wa Mungu. Hata hivyo, Askofu Lai alijibu ujumbe wangu saa tano asubuhi, wakati ambapo tayari nilikuwa nimehudhuria hafla ya utalii. Ingawa nilichelewa, nilisisitiza kwamba kwa vyovyote vile, lazima nifike JCC. Nilipowasili saa tano asubuhi, aliniarifu kuwa ibada kuu ilikuwa imeisha lakini akasema kuwa kuna ibada ya kifamilia kuanzia saa tisa na nusu mchana,” aliongeza.

Rais Ruto alisisitiza kuwa alikuwa amedhamiria kuhudhuria ibada hiyo licha ya kufika akiwa amechelewa.

“Niliamua moyoni mwangu kwamba lazima nifike JCC na kusikiliza mahubiri. Nilimweleza Askofu kuwa ningeenda kumaliza majukumu yangu kisha nirudi baadaye jioni. Namshukuru Mungu kuwa niliweza kuhudhuria ibada hii. Imekuwa muda mrefu tangu nilipokuja hapa kumsikiliza Askofu Lai,” alisema.

Kiongozi huyo wa taifa alimshukuru Askofu Lai kwa kuhubiri kwa hekima na kusema ukweli kuhusu hali ya taifa na uongozi wake, huku akiwaomba waumini waendelee kuombea nchi.

“Askofu ameongea kwa hekima na ukweli kuhusu taifa letu na uongozi wake. Nimefurahi na kubarikiwa sana. Kama ulivyosema, Askofu, Mungu anaponya taifa na uchumi wetu. Nitakuwa Pwani kwa wiki moja nikisimamia miradi ya maendeleo katika eneo hili. Namshukuru Mungu kwa fursa ya kuwa hapa leo,” alisema.

Rais Ruto, anayejulikana kuhudhuria ibada za kanisa kila Jumapili asubuhi alikosa kuhudhuria ibada kuu Februari, 23.

Kama si kwa ibada ya kifamilia inayofanyika kuanzia saa tisa nchana katika JCC, Rais angekosa kabisa kuhudhuria ibada Jumapili hiyo.

Rais alipowasili kanisani siku hiyo asubuhi, alikuta ibada kuu ikiwa imeisha na kulazimika kuondoka kwa muda, lakini baadaye alirejea jioni kueleza sababu ya kuchelewa kwake.

Alimshukuru Askofu Lai na kueleza imani yake kuwa kila kitu kitafanyika kulingana na mpango wa Mungu. Alisisitiza kuwa ziara yake Pwani imelenga kuzindua miradi ya maendeleo ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

“Ninakubaliana nawe, Askofu, kwamba kile ambacho Mungu amepanga hakuna mwanadamu anayeweza kupangua. Hivyo basi, nawaomba muendelee kutuombea,” alisema, akishangiliwa na waumini.

Rais Ruto, ambaye ameimarisha sifa yake kama ‘Mkristo mwaminifu’ na kawaida huanza Jumapili zake kwa ibada, alikuwa na asubuhi yenye shughuli nyingi, jambo lililosababisha tukio hilo nadra.

Siku yake ilianza katika Bandari ya Mombasa, ambako aliikaribisha rasmi meli ya kifahari ya MS Norwegian Dawn, iliyokuwa na watalii zaidi ya 2,200.

Rais alitumia muda wake kuwapokea wageni hao, akisisitiza dhamira ya Kenya ya kupanua sekta ya utalii na kuimarisha sifa yake kama kivutio bora cha watalii.

Alieleza kuwa serikali yake itawekeza katika miundomsingi, kutekeleza mikakati madhubuti ya masoko, na kuboresha huduma za utalii ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea nchi.

Katika hafla hiyo, Rais aliandamana na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir, Waziri wa Utalii Rebecca Miano, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (KPA), Kapteni William Ruto, miongoni mwa viongozi wengine.

Meli hiyo yenye urefu wa mita 294, inayoongozwa na nahodha Maxim Kyselov, ni miongoni mwa meli ndefu zaidi zilizotia nanga katika bandari ya Mombasa mwaka huu.

Baada ya shughuli hiyo bandarini, Rais alielekea JCC, lakini kuchelewa kwake kulishangaza wengi, kwani anajulikana kurauka katika ibada za kanisa.

Licha ya kukosa ibada kuu, Rais alitumia muda kuzungumza na baadhi ya waumini waliokuwa bado kanisani baada ya ibada. Pia alipata nafasi ya kuzungumza kwa kifupi na Askofu Lai kabla ya kuendelea na ratiba yake ya siku. Baadaye jioni, alirejea kanisani kumaliza Jumapili yake kwa ibada.

Rais Ruto yuko Pwani kwa ziara ya kikazi ambapo anatarajiwa kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile uwekaji jiwe la msingi kwa ujenzi wa Shule ya Upili ya Kiwegu na mradi wa kuunganisha umeme katika shule hiyo huko Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale.

Pia, anatarijiwa kuzindua mradi wa kuboresha Kituo cha Afya cha Mkongani hadi hadhi ya hospitali ya Kaunti Ndogo, Kuzindua chumba cha upasuaji na wodi ya wagonjwa katika Hospitali ya Mkongani, Matuga.

Rais Ruto pia anatarajiwa kugawa hati miliki za ardhi na kuweka jiwe la msingi kwa mradi wa nyumba za bei nafuu katika eneo la Whitehouse, Ukunda.