Habari

Murkomen asema miili haijapatikana licha ya kuthibitisha 20 wametoweka mpakani Turkana

Na SAMMY LUTTA February 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ZAIDI ya watu 20 wameripotiwa kutoweka kutokana na kisa cha uvamizi kinachodaiwa kutekelezwa na wapiganaji wa Dassenech kutoka Ethiopia dhidi ya wavuvi wa Turkana.

Uvamizi huo ulitokea mnamo Jumamosi katika kijiji cha Lopeimukat kwenye mpaka wa Kenya-Ethiopia na maafisa wa serikali wamethibitisha kutoweka kwa Wakenya hao.

Naibu Kamishna wa Turkana Kaskazini, George Orina, alithibitisha kutoweka kwa watu hao ambao inahofiwa wameuawa na jamii ya Dassenech.

Bw Orina alikuwa kwenye ujumbe wa Kenya uliojumuisha maafisa wa serikali kuu, viongozi wa kisiasa na wale wa Kaunti ya Turkana ambao walijaribu kufika Ziwa Turkana lakini hawakufanikiwa huku wakipokezwa tu maelezo na manusura.

“Hadi sasa boti 16, bunduki moja na pikipiki moja zimepatikana. Watu 22 wakiwemo wafugaji wa kuhamahama na wavuvi bado wametoweka wala hawajapatikana,” akasema Bw Orina.

Vyombo vya usalama viliandaa mkutano wa usalama pamoja na wenzao wa Ethiopia mnamo Jumapili na wakaweka mikakati ya jinsi watakavyofaulu kuondoa miili ya wanaodaiwa kuuawa au kuwaokoa manusura.

“Tuliacha mifuko ya kuweka miili ili itumike iwapo mingine itapatikana kabla ya kurejelea oparesheni Jumatatu,” akasema.

Kikosi cha Msalaba Mwekundu nacho kilikuwa nyanjani kutoa ushauri nasaha kwa manusura ambao waliathirika na shambulio hilo kisaikolojia.

Kwa mujibu wa Chifu ya Lokesheni ya Todonyang Eraman Ekale, mzozo ulianza wakati ambapo wanaume waliojihami kutoka Turkana waliwapiga risasi watu watatu kutoka jamii ya Dassenech/Merille eneo la Nang’orikitoe katika mazingira ya kutatanisha.

“Kama njia ya kulipiza kisasa jamii ya Dassenech waliwaendea wavuvi Wakenya eneo la Lopeimakamate na Cess ambao hawakuwa na habari kuhusu mauaji hayo,

“Kufikia saa 11 jioni, niliambiwa kuwa kulikuwa na boti saba eneo la Lopeimukat lakini waliokuwa ndani walikosekana. Bado hatujathibitisha vifo hivyo,” akasema Bw Ekale.

Maafisa wa usalama kwa zaidi ya saa 20 hawakuwa wamebaini idadi ya watu ambao walikuwa wameuawa au waliokuwa wametoweka.

“Hatungeweza kufika eneo la tukio kwa sababu ya taharuki na pia ziwa limefurika. Tumeungana na walinda usalama na kamati husika za kiusalama ili tuelekee eneo ambapo watu hao wanadaiwa kutowekea,” akasema Bw Orina.

Haya yanaendelea wakati ambapo Mbunge wa Turkana ya Kaskazini Ekwom Nabuin na mwenzake wa Turkana Kusini Dkt Ariko Namoit wamedai kuwa zaidi ya Waturkana 20 wameuawa kwenye uvamizi huo.

“Tumepokea habari za kusikitisha kuwa zaidi ya wavuvi 20 wameuawa kinyama eneo la Todonyang’ Ziwa Turkana na jamii ya Dassanech kutoka Ethiopia. Idadi kamili huenda ikawa juu,” akaandika kwenye mtandao wake wa kijamii.

“Mauaji hayo yanatokea kwenye ardhi ya Kenya ambayo imekaliwa na wapiganiaji waliojihami wa Ethiopia kutoka kwa jamii ya Dassanech,” akaongeza.

Dkt Namoit naye alisema serikali lazima ichukue jukumu lake la kikatiba kulinda maisha ya raia na mali yao.

Alisema mauaji hayo yanaendelea kuvuruga amani mpakani na akamtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen aingilie kati na kuwaokoa wengine ambao alidai bado wametoweka.

Gavana Jeremiah Lomorukai, wabunge Protus Akuja (Loima) Emathe Namuar (Turkana ya Kati) na Mbunge Mwakilishi wa Kike Cecilia Ngitit wote wamelaani mauaji hayo wakisema serikali kuu ingehakikisha usalama mpakani basi hayangetokea.