Habari

Wanafunzi wawili wa chuo cha KMTC wafa maji wakiogelea baharini

Na WACHIRA MWANGI February 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WANAFUNZI wawili wa Chuo cha Mafunzo ya Matibabu Kenya (KMTC) tawi la Mombasa, walipoteza maisha baada ya kuzama Jumatatu asubuhi walipokuwa wakiogelea baharini.

Baada ya mwili wa mwanafunzi mmoja mwenye umri wa miaka 22 kupatikana, juhudi za kumsaka mwathiriwa wa pili (26) zilikuwa zinaendelea.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka kwa Huduma ya Walinzi wa Pwani za Kenya (KCGS), wanafunzi hao wawili walikuwa sehemu ya kundi lililokuwa likicheza mpira ufuoni kabla kisa hicho kutokea.

Kulingana na walioshuhudia, wanafunzi hao walikuwa wakicheza kandanda kabla ya kuingia baharini kuogelea.

Kwa bahati mbaya, mawimbi makali yaliwazidi nguvu na kuwazamisha majini.

Maafisa wa KCGS, kwa kushirikiana na mashirika mengine ya uokoaji, walianzisha msako kutafuta miili hiyo.