Taarifa za kuuawa kwa polisi Haiti zafikishwa kijijini kwao Kajiado na kuacha simanzi kuu
HALI ya huzuni imetanda katika kijiji cha Naserian katika Kaunti ndogo ya Kajiado Mashariki kufuatia taarifa kuhusu kifo cha afisa wa polisi aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiwa kazini nchini Haiti siku ya Jumapili.
Taarifa ya kufariki kwa Samuel Tompei Kaetuai, 28, zilifikishwa kijijini humo na maafisa wa polisi Jumatatu asubuhi na kuacha kijiji kizima na huzuni tele.
Babake marehemu Bw Kaetuai Lesarumba aliyejawa na majonzi alimtaja afisa huyo ambaye alikuwa akihudumu katika kitengo cha polisi cha kupiga doria mipakani kuwa mtu aliyetegemewa kwani alikuwa mtu wa pekee ambaye alikuwa ameajiriwa katika familia na kusema kifo chake ni pigo kubwa kwa familia hiyo.
“Tumepokea habari za kifo chake kwa huzuni. Naomba serikali ilete mwili wake nyumbani nipate kuamini ni yeye. Familia yote ilikuwa na matumaini makubwa kwake,” alisema babake marehemu.
Marehemu amemwacha mjane Naomi Samuel wa umri wa miaka 23 na watoto wawili wachanga. Mjane alisema alikuwa akiwasiliana na mumwewe kupitia jumbe za simu.
“Sikuweza kuongea naye kwa simu hivi karibuni lakini alikuwa anatuma ujumbe kila siku akitaka kujua hali yangu na watoto,” alisema Bi Naomi.
Msemaji wa familia Bw Joseph Kimiti alisema kifo cha afisa huo wa polisi ni pigo kubwa kwa familia na jamii nzima kwa jumla.
“Ni huzuni kubwa kumpoteza kijana ambaye tulitegemea atawasaidia wazazi na jamii. Alipopata kazi tulijua atakuwa mfano mwema kwa vijana huku kijinini,” aliongezea.
Marehemu alikuwa akihudumu katika kitengo cha kupiga doria mipakani katika kaunti za Mandera na Wajir tangu mwaka 2021 kabla ya kuelekea nchini Haiti.
Kifo hicho kimezima ndoto nyingi alizokuwa nazo maishani, mawe ya kujenga nyumba yakisalia kumbukumbu ya safari aliyopania kuanza kubadilisha maisha ya familia yake.
Serikali imetoa taarifa kuhusu kifo cha afisa huyo, ila haijaeleza mipango ya kusafirisha mwili wake hadi nyumbani kwa hafla ya mazishi.