Raila njoo nikupe urais – Gachagua
ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua sasa anasema kwamba anaweza kumfanya kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwa rais wa Kenya iwapo atakubali kuungana naye na vigogo wengine wa upinzani.
Bw Gachagua anasema kwamba wapigakura wa Mlima Kenya wako tayari kumuunga mkono Bw Odinga kumshinda Rais Ruto katika kura za 2027.
Ili kufanikisha hili, Bw Gachagua alidai kuwa anashauriana mara kwa mara na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta kuhusu suala hilo, akidai ni Bw Odinga pekee ndiye anajivuta kukubali.
“Kama mkubwa wangu katika mpangilio wa wazee, Bw Kenyatta hutushauri wakati wowote tunapokuwa na hitaji… tunapotembea katika safari hii, yuko pamoja nasi,” Bw Gachagua alidai katika mahojiano ya KTN, Jumatatu usiku.
Bw Gachagua alisema ni juu ya Bw Odinga kuamua ikiwa anataka kuungana na Ruto au kukumbatia Mlima Kenya “na kufanywa rais”.
Alimkumbusha Bw Odinga kwamba “sisi katika eneo la Mlima Kenya tumeonyesha kuwa tunaweza kumuunga mkono mtu wa nje ya jamii yetu ikizingatiwa kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 tulimpa Ruto asilimia 87 ya kura zetu na zilizosalia zikaenda kwako (Raila)”.
“Ni juu yake kuamua kama anataka kuwa rais. Kwa sasa ni mapema kulizungumzia. Hakuna jinsi anaweza kuungwa mkono bila yeye kuamua kwanza,” Bw Gachagua alisema.
Bw Gachagua alisema kwa sasa anaunda muungano wa kumpinga Rais Ruto 2027 na “mimi mwenyewe, Odinga, (Kiongozi wa Wiper) Kalonzo Musyoka, (Gavana) George Natembeya, (Seneta) Okiya Omtatah, (kiongozi wa DAP) Eugene Wamalwa” miongoni mwa wengine wanaotarajiwa kugombea urais.
“Bw Musyoka anafaa… Bw Odinga kama mgombeaji wetu wa urais anasisimua zaidi. Huwa anapata takriban kura milioni sita kwa wastani, sisi tuna milioni sita. Kufikia saa nne asubuhi ya siku ya kupiga kura, Rais Odinga atakuwa amepatikana,” Bw Gachagua alidai.
Bw Gachagua alisema wabunge wa chama cha ODM anachoongoza Bw Odinga hawakufanya lolote baya kumsaidia Rais Ruto kumuondoa yeye mamlakani kama naibu rais.
“Ni Rais Ruto ndiye aliyepanga kutimuliwa kwangu. Yeye ndiye adui yetu mkuu na ndiye pekee ambaye amefungiwa nje ya mazungumzo yoyote ya ushirikiano na Mlima Kenya,” akaeleza.
Lakini msimamo wa hivi punde wa Bw Gachagua kuhusu Bw Odinga unakinzana na ule wa mshirika wake, Seneta wa Nyandarua, Bw John Methu.
“Walipomtimua Bw Gachagua walisherehekea na sasa ni wakati wetu wa kusherehekea chochote kinachowaumiza Ruto na Odinga,” Bw Methu alisema katika Kaunti ya Meru, Jumapili iliyopita.
Bw Odinga amewataka wafuasi wake kuwa na subira anaposhauriana kuhusu mwelekeo ujao wa kisiasa baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).
Bw Gachagua alidai Rais Ruto anataka kumdanganya Bw Odinga kwa cheo ambacho hakipo cha Waziri Mkuu.
“Huwezi kujaribu kuwa rais mara tano kisha ujidunishe kuwa Waziri Mkuu? Shinda urais,” Bw Gachagua akamsihi Bw Odinga, 80.
“Ikiwa Ruto sasa anaamini wewe si kuhani wa umaskini tena, kwamba wewe ndiwe bora zaidi kwa Afrika hadi akawa anakupigia kampeni ili uwe mwenyekiti wa AUC, acha atangaze kwamba atafanya muhula mmoja na kukuidhinisha wewe kumrithi 2027,” mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema.
Naibu huyo wa rais wa zamani alisema Mlima Kenya sasa umejifunza kwa njia ngumu kwamba kwa muda wote huo umemfanya Bw Odinga kuwa adui katika uchaguzi bila sababu.
“Wakati mwingine mimi hulia faraghani kwa masikitiko jinsi Ruto alivyonilaghai, kunihadaa na kufanya kampeni yenye ukora (Mlima Kenya),” alidai.
“Tumekuwa tukiingia katika uchaguzi tukiwa na dhana potovu kwamba Bw Odinga ni mtu mbaya ambaye ni mzuri tu katika machafuko na kukuza umaskini. Lakini sasa tuna hekima zaidi na tuko tayari kuungana naye,” akasema.
Akilenga wafuasi wa Bw Odinga, Bw Gachagua alisema: “Sisi si maadui. Tuna tatizo tu na Rais Ruto, si Odinga, jamii yake, wafuasi wake au ODM.”
Alisema Mlima Kenya haukuwa ‘mpigakura’ katika uchaguzi wa AUC “na ukweli kwamba watu wetu wachache walionekana wakisherehekea kushindwa kwake haimaanishi kuwa eneo hilo halikuunga azima yake”.
Seneta wa Murang’a, Bw Joe Nyutu, Mbunge wa Maragua Mary wa Maua na Seneta wa Kisii Bw Richard Onyonka walisema Bw Odinga anafaa kuzingatia mwaliko wa Bw Gachagua. Lakini Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Kimani Ichung’wa, Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri na Mbunge wa Kapseret, Bw Oscar Sudi walipuuza kauli za Bw Gachagua.
Bw Nyutu aliambia Taifa Leo, “Tunaunga mkono kikamilifu mfalme wetu kutoka Wamunyoro.”
“Kabla ya kwenda kwa mahojiano alikuwa ametuuliza maoni yetu, tulimweleza kuwa tunakubaliana kwamba tuko tayari kufanya kazi na yeyote isipokuwa Ruto mwenyewe,” Bw Nyutu alisema.
Wa Maua alisema, “Tunamuunga mkono Bw Gachagua katika harakati zake za ustawi wa nchi na tumemuagiza kufanya kazi na viongozi wote wanaoitakia nchi hii mema.”
“Siku zimepita ambazo sisi kama Mlima Kenya tulishiriki uchaguzi kwa chuki isiyo na msingi. Sasa tuko tayari zaidi kumuunga mkono mgombeaji yeyote ambaye anaweza kutufanya kutazama upya ndoto ya ustawi ya mababu zetu,” aliongeza.
Bw Onyonka Jumanne aliambia Taifa Leo kwamba Bw Odinga anafaa kumchukulia Bw Gachagua kwa uzito.
“Bw Odinga anafaa kufuata ushauri wa Wamunyoro. Bw Odinga anapaswa kuwa mwangalifu sana na Rais Ruto. Kwa kumwahidi Bw Odinga nafasi ya Waziri Mkuu, ni upumbavu kwa vile itahitaji kura ya maamuzi,” Bw Onyonka aliteta.
Katibu Mkuu wa ODM Bw Edwin Sifuna aliambia runinga ya Citizen “jinsi Rais Ruto anavyowaogopa watu wa Kenya hawezi kutamani kuwakabili wananchi kwenye kura ya maamuzi.”
Bw Odinga, aliendelea, haitaji ushauri wowote ambao hajaomba, na kuongeza “sisi kama chama tunajua Bw Odinga ana akili na sauti yake iko sawa na ikihitajika aeleze hisia zake kuhusu 2027, atazungumza mwenyewe”.
Lakini Bw Kiunjuri alisema Bw Gachagua amekuwa mtu wa kutoa misimamo kinzani.
“Hauwezi kutuambia kwamba unaunganisha Mlima Kenya ili kumchukia Rais Ruto na kutarajia tukuchukulie kwa uzito. Kinachomsukuma Bw Gachagua ni hasira, kisasi na ubinafsi unaofanya achukulie wapiga kura wa Mlima Kenya kama bidhaa zake kufanya biashara sokoni,” Bw Kiunjuri alisema.
“Rekodi ziko wazi kuhusu mambo mengi mabaya ambayo amesema kuhusu Bw Odinga. Sisi si wajinga kutojua kwamba anaunga mkono Bw Odinga na Mahakama ya Juu ili kupata manufaa ya kibinafsi. Bw Gachagua hawezi kuwa mtu wa kuokoa Kenya na Bw Odinga,” Bw Kiunjuri alidai.