Ruto aahidi kushirikiana na Raila uchaguzi mdogo wa Magarini
RAIS William Ruto ameahidi kuhakikisha kiti cha Magarini kitanyakuliwa na mgombeaji ambaye wataamua pamoja na kinara wa ODM Bw Raila Odinga uchaguzi mdogo utakapofanyika.
Rais Ruto alisema atahakikisha kiti hicho hakinyakuliwi na wapinzani wake na wa Bw Odinga.
Kiti hicho cha ubunge kilibaki wazi miaka miwili iliyopita baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali uchaguzi wa Bw Harrison Kombe wa ODM.
Rais Ruto alisema atahakikisha wapinzani wake ambao wanamezea mate kiti hicho hawakipati. “Hasidi hawatapata nafasi ya kupenya,” alisema Rais Ruto kwenye mazishi ya babake Spika wa Bunge la Seneti, Bw Amason Kingi, marehemu Mzee Kingi Mwaruwa Mkweha huko Kilifi.
Mnamo Mei 2024, Majaji watano wa Mahakama ya Juu walisema mpinzani wa Bw Kombe, Stanley Kenga alidhibitisha kesi hiyo.
Bw Kenga, ambaye alikuwa Naibu wa Spika wa Bunge la Kilifi aligombea kiti hicho, kupitia chama cha UDA na kuzoa kura 11, 925 huku mpinzani wake (Bw Kombe) akipata kura 11, 946 (ODM).
Rais alisema atakita kambi eneo la Pwani ili kuzindua miradi mbali mbali na kutatua changamoto za wapwani.
“Niko hapa kuhakikisha Pwani ambayo imebaki nyuma inapata maendeleo sawia na sehemu zingine nchini, nitakuwa hapa kuzindua miradi ya nyumba, soko, barabara na zengine,” aliongeza.
Rais alisema Serikali inapania kununua ardhi kutoka kwa wamiliki wa ardhi wasioishi nchini na kuwahamishia wakazi wasio na makazi rasmi katika ukanda wa Pwani.
Rais William Ruto alitangaza kuwa tayari amemkabidhi Spika wa Seneti Amason Kingi, Waziri Hassan Joho (Madini) na Waziri Salim Mvurya (Michezo) jukumu la kutambua na kuhakiki wamiliki halali wa ardhi wasioishi nchini kwa ajili ya fidia.
“Tumepiga hatua, na sasa tunazo fedha za kuwalipa hawa wamiliki wa ardhi wasioishi nchini,” alisema wakati wa ibada ya mazishi ya baba yake Kingi, Mzee Kingi Mwaruwa Mkweha, huko Kamale, Kaunti ya Kilifi.
Kwa mujibu wake, hii ni hatua ya kwanza katika kutatua changamoto za ardhi za kihistoria ambazo zimeikumba Pwani kwa karne nyingi, na kuwaacha maelfu ya wakazi bila hati miliki za ardhi.
Aidha alikiri kuwa sio jambo la rahisi na litachukua muda kulitimiza.