Maoni

MAONI: Kalonzo yaonekana haamini Raila sasa ni mshirika serikalini, harudi upinzani

Na KINYUA KING'ORI February 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

UOGA wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ndio unaochangia kuonekana kutishika na hatua ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuamua kushirikiana na Rais William Ruto baada ya kufeli AUC majuzi.

Sikumbuki hata siku moja Bw Kalonzo ambaye ni mwanasiasa mkongwe mwenye tajriba pevu, akijihusisha kikamilifu na ufanisi huo. Licha ya Bw Kalonzo kuwa katika upinzani kwa kipindi kirefu, bado hajathibitisha ujasiri wa kupigania haki za Wakenya na kutekeleza majukumu ya upinzani bila uwepo wa Bw Odinga.

Amefeli kutumia mafanikio aliyowezesha serikalini kushabikiwa na Wakenya wala hakuna dalili ya kuthibitisha atafaulu katika uchaguzi wa mwaka wa 2027.

Bw Kalonzo anafaa kusahau ushirikiano na Bw Odinga 2027 maana amethibitisha kuwe usiku au mchana ataendeleza ukuruba wake na Rais Ruto.

Ikiwa Bw Kalonzo anajiamini alitekeleza wajibu wake kuongoza upinzani vyema kama alivyodai juzi, mbona aendelee kubembeleza Raila kujiunga naye kupiga jeki azma yake badala ya kuendelea kujitokeza kupigania haki za Wakenya akijipanga kisiasa bila kuogopa vitisho vya wapinzani wake wanaomkejeli ili kuhujumu azma yake 2027.

Pia anafaa kutumia mbinu alizotumia kuhakikisha jamii yake Ukambani inamuunga mkono kushawishi Wakenya wampigie kura 2027, badala ya kutumia muda mwingi kufikiria kuungwa mkono na Raila anayeonekana kumsaliti licha ya kuwa mgombeaji mwenza katika chaguzi za 2013 na 2017.

Asuke mbinu kuimarisha mahusiano yake na wapigakura bila kuzingatia kabila.

Ukweli ni kwamba Bw Kalonzo ni kiongozi mpole, mtulivu na mzoefu anayeweza kuleta mabadiliko katika taifa hili hasa kiuchumi na kiustawi akichaguliwa.