Jinsi raia wa UG walivamia boma Busia, wakaua vijana wawili na kutupa miili mtoni
FAMILIA mmoja katika Kaunti ya Busia inalilia haki baada ya watoto wao wawili kuuawa na watu wanaotoka Uganda kwa madai ya kuteketeza nyumba 20 na kuwakata ng’ombe saba kisha kuvukia upande wa Kenya.
Mama Susan Akuru kutoka kijiji cha Mong’odewa Lokesheni ya Apokor, Moding, Kaunti ya Busia, anasaka haki kutokana na mauaji ya wanawe Paul Amukaga na Stanley Opidi mnamo Februari 12.
Wawili hao wamekuwa wakimsaidia Bi Akuru na ndugu yake Michael Opidi kupasua mawe ya kutengeneza kokoto na siku hiyo walikuwa katika shughuli yao kama kawaida.
Hata hivyo, baada ya chamcha, vijana waliopandwa na mori walivamia boma lao la kuwachukua Mabw Opidi na Amukaga wakiwashutumu kwa kuwakata ng’ombe saba na kuteketeza nyumba 20 Uganda.
“Hawakutaka kumsikiza mtu yeyote na nilipowauliza kosa gani watoto wangu walikuwa wametenda, walitishia kuniadhibu kwa kuwalea watoto wasiokuwa na maadili.
“Waliwaburura wanangu nje ya lango letu ambako chifu wetu Gilbert Odera alikuwa akiwasubiri,” akasema Bi Akuru.
Alipomuuliza chifu kuhusu kilichokuwa kikiendelea, Bw Odera aliamuru wanawe wafungwe kwa kamba miguuni kisha wakawekwa kwenye pikipiki na wakaondoka nao.
“Nilijua walikuwa kwenye mikono salama ya chifu na kuwa walikuwa wakipelekwa kwenye kituo cha polisi. Nilienda kuoga ndipo nikaenda katika kituo cha polisi lakini nikashtuka kuambiwa hawakuwa hapo wala polisi hawakufahamu chochote kuhusu tukio hilo,” akasema.
Alipokuwa akirudi nyumbani, alikumbana na dadake Beatrice Akisa ambaye alimfahamisha jinsi wanawe waliuawa kinyama kwenye Mto Lwakhakha.
“Sikuamini kile ambacho nilikuwa naambiwa. Ni kama ulimwengu ulikuwa unaisha na ilikuwa vigumu kukubali kile ambacho nilikuwa naambiwa,” akasema huku akidondokwa na machozi.
Familia hiyo inaamini kuwa Chifu Odera aliwasindikiza vijana hao hadi mtoni kisha kuwakabidhi kwa wanakijiji waliojawa na hasira kutoka Uganda.
“Chifu alitumia pikipiki moja huku nyingine iliyombeba Amukanga ikiendeshwa na kijana mmoja kutoka kijiji chetu. Chifu na vijana waliwakabidhi vijana hao kwa raia wa Uganda kwenye ukingo wa Mto Lwakhakha kwenye ardhi ya Kenya,” akasema Bi Akisa.
Kwa machungu alisimulia kuwa vijana hao w waliwapiga wanawe, wakawakata kichwa na shingo kisha baada ya kuwaua waliwatupa mtoni.
“Mmoja wa hao wanakijiji aliteka maji ambayo yalikuwa na damu kisha akayanywa. Ni tukio la kusikitisha,” akasema.
Chifu Odera naye alisema alijaribu kuwaokoa vijana hao kutoka kwa raia wa Uganda lakini akalemewa. Alijiondolea lawama kuwa alishirikiana nao kuhakikisha vijana hao wameuawa.
“Nilifahamishwa kuwa wanakijiji kutoka Uganda walikuwa wamevamia lokesheni yangu kuwachukua watu waliokuwa wanashukiwa kuwa wahalifu. Nilikimbia na kabla nifike kwenye boma hilo nilipata vijana hao wakivutwa. Niliuliza nini ilikuwa ikiendelea na wakanipuuza,” akasema Bw Odera.
Chifu huyo alisema wenzake wa Uganda walimwambia vijana hao walichoma nyumba na kuwakata ngómbe mnamo Februari 11 kabla ya kuvukia upande wa Kenya kwa mama wao.
Hata hivyo, Bi Akuru amekanusha hilo akisema wanawe wamekuwa wakiishi naye tangu Disemba 19 walipotoka kwa baba yao anayeishi Uganda ambaye alikuwa mumewe lakini wakatengana.