Habari za Kitaifa

Wasiwasi watu wanaokumbwa na matatizo ya afya ya kiakili wakiongezeka Kenya

Na  WAIKWA MAINA March 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DATA kutoka kwa Wizara ya Afya inaonyesha kuwa idadi ya watu wanaokumbwa na matatizo ya afya ya kiakili imeongezeka.

Kulingana na data hiyo, kaunti nyingi zimerekodi ongezeko la magonjwa ya akili katika miaka mitatu iliyopita.

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya 2022 na 2023, idadi ya watu waliokuwa wakipambana na afya ya kiakili iliongezeka kutoka 171,845 hadi 184,292.

Kaunti zilizokuwa na idadi kubwa ya kesi 2024 zilijumuisha Nairobi 53,521, Murang’a 9,607, Nakuru 8,633, Machakos 6,648, Kiambu 6,500 na Nyeri 6,497.

Kwa upande mwingine, idadi hizo zilipungua katika kaunti za Mandera na Marsabit.

Mandera ilikuwa na idadi ndogo zaidi ya 264 mwaka 2024 kutoka 633 mwaka wa 2023, huku Marsabit ikirekodi kesi 323 ikilinganishwa na 337 mwaka wa 2023.

Dkt Sarah Bahati, daktari mshauri wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Nyahururu Level Four anasema masuala ya afya ya akili yanaongezeka kutokana na mafadhaiko yanayoongezeka kama vile changamoto za kiuchumi na shinikizo la kijamii.

‘Kati ya watu wanne, angalau mmoja ana shida ya afya ya kiakili. Katika hospitali, mmoja kati ya kila wagonjwa wana mfadhaiko au ugonjwa mwingine wa akili,” asema.

Licha ya wasiwasi unaoongezeka unaotolewa na wataalamu na washikadau wa afya ya akili, ripoti kadhaa zilizo na mapendekezo yanayoweza kutekelezewa ya kuzuia na kupunguza matatizo ya akili bado hazijatekelezwa.

Ni pamoja na ripoti ya Afya ya Akili Jopo Kazi  la Kenya kuhusu Afya ya Akili, kilichoanzishwa mwaka wa 2019 na Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.

Kikosi kazi kiliwasilisha matokeo na mapendekezo yake kwa serikali mnamo Julai 2020.

Miongoni mwa mapendekezo ya dharura kutoka kwa ripoti ya kikosi kazi ni kujumuisha afya ya akili katika huduma ya afya ya msingi, kutoa mafunzo kwa watoa huduma ili kudhibiti hali za kawaida za afya ya akili, kutangaza afya ya akili kuwa la dharura, na kuboresha ukusanyaji wa data na utafiti.

Jopokazi hilo pia lilipendekeza kuanzishwa kwa Tume ya Kitaifa ya Afya ya Akili ili kufuatilia maendeleo, kutoa ushauri kuhusu sera, na kuratibu programu za afya ya akili nchini kote.