Sitasahau raia katika tangazo kuhusu mwelekeo wangu wa kisiasa, asema Raila
KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga ameshikilia kuwa hatua atakayochukua na kutangaza wiki ijayo itakuwa ya manufaa ya Wakenya wote.
Aliwaacha Wakenya wakikisia kuhusu hatua yake inayofuata baada ya kushikilia kuwa ataendelea na mashauriano yake kabla ya kutangaza mwelekeo wake ujao.
Bw Odinga, ambaye maoni yake yamezua uvumi kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa, alisema kuwa chama chake kitaendelea kupigania haki za Wakenya.
Bw Odinga alitoa kauli hiyo huku kukiwa na wasiwasi miongoni mwa washirika na wafuasi wake kwamba ataachana na mapambano ya utawala bora kwa kumkumbatia Rais William Ruto ambaye analaumiwa kwa kuelekeza nchi pabaya.
“Nitaendelea kushauriana ili kuhakikisha kwamba tunachukua mwelekeo utakaotanguliza mahitaji na haki za Wakenya. Hatutakuwa na mzaha,” alisema Bw Odinga.
Kiongozi huyo wa ODM alikuwa akizungumza huko Funyula, Kaunti ya Busia jana, wakati wa kuadhimisha miaka 20 ya chama hicho.
Alisema chama hicho kitahifadhi maadili yake ya kutetea raia.
Pia alisema anajua anachofanya, akisema Chama cha ODM hufanya maamuzi baada ya kufikiria kwa kina.
“Chama chetu kina mwelekeo. Hatuwafuati watu kwa upofu na bila mpango, tunafanya hivyo kwa sababu. ODM ina maadili yake na tutaendelea kupigania haki na maslahi ya raia.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa chama hicho akiwemo Kaimu Kiongozi Prof Anyang’ Nyong’o, Naibu Viongozi watatu wa Chama Gavana Simba Arati, Abdulswamad Nassir, Godfrey Osotsi, Mwenyekiti Gladys Wanga na Katibu Mkuu Edwin Sifuna.
Bw Odinga alitoa hakikisho hilo huku chama chake kikimwachilia rasmi ili kushirikiana na serikali, kikiahidi kumfuata popote atakapokielekeza.
Bi Wanga alisema katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, chama hicho kimefanikiwa kusalia imara kutokana na uongozi wa Bw Odinga.
“Raila kwa sasa anafanya mashauriano kote nchini. Ukimaliza tutafuata chochote utakachosema, ukisema twende kushoto au kulia tutafuata,” alisema.
Maoni yake yaliungwa mkono na Bw Arati ambaye, alitambua jukumu la Rais Ruto wakati wa kampeni za Tume ya Muungano wa Afrika, na kusema chama hicho kinajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.
“Kama chama, lazima tuchukue uongozi. Tumejiandaa kwa 2027. Kwa njia yoyote, sisi wenyewe au kwa njia ya muungano, lazima tuchukue uongozi wa nchi hii,” alisema.
Alimtaka Bw Odinga kuendelea na mashauriano yake na kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa waathiriwa wa ukatili wa polisi. Aliwaonya wanachama wa chama hicho ambao alisema walikuwa na tabia ya kukosa heshima.
“Kama naibu kiongozi wa chama, ninamfuata Bw Odinga. Tutashughulikia wale ambao hawana heshima. Ninaomba tushikane mikono na kusonga mbele,” akasema.
Wakati huo huo, Bw Sifuna na Gavana wa Siaya James Orengo waliwatahadharisha wanachama wa chama hicho kuwa waangalifu ili wasipoteze chama chao.
“Tunataka ODM iendelee kuwa chama chenye nguvu zaidi. Ni chama kikubwa kwa sababu ya Raila Amollo Odinga ambaye ana msimamo kuhusu masuala. ODM ni chama chenye utambulisho, manifesto na chenye mwelekeo. Ninawaomba wanachama wote kusalia imara na kutoruhusu chama kipoteze utambulisho wake kama vuguvugu la kimaendeleo,” akasema Bw Orengo.
Sawa na Bw Arati, alisisitiza kuwa ODM lazima itwae mamlaka humu nchini kupitia uchaguzi. “Tuna itikadi na mwelekeo. ODM lazima iongoze na haiwezi kumezwa, ni chama cha kumeza vingine,” akasema Bw Orengo.
Kiongozi wa Chama cha Roots George Wajackoyah ambaye pia alikuwepo alisema ni wakati muafaka Wakenya kujua kwamba mabadiliko yanakuja hivi karibuni.
Aliapa kuambatana na Bw Odinga huku washirika wake wa zamani wakiendelea kuungana na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Bw Junet Mohamed alisema kuwa huku vyama vingine vikiendelea kuzozana, ODM imesalia imara na daima kitakuwa chama kinachotetea raia.