Maaskofu wakemea wanasiasa kwa kampeni za mapema za uchaguzi wa 2027
MAASKOFU wa Kanisa Katoliki wamewataka wanasiasa kusitisha kampeni za uchaguzi kabla ya wakati, wakionya kwamba wanaweza kugeuza mawazo ya kitaifa kutoka kwa masuala muhimu.
Ikiwa imesalia zaidi ya miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu maaskofu hao wameibua wasiwasi kuhusu hali ya kisiasa ambayo tayari inazidi kupamba moto, na kuwataka viongozi kutanguliza utawala, vita dhidi ya ufisadi, usalama na kupanda kwa gharama ya maisha.
Wakizungumza mjini Mombasa wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Kwaresima 2025 katika eneo la Mama Ngina Waterfront, Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki nchini (KCCB) lilisema kampeni za mapema zinazidisha mivutano ya kisiasa nchini.
“Kuanza mapema kwa kampeni kunaondoa umakini kutoka kwa maendeleo ya kitaifa, kuelekeza umakini katika siasa huku utawala ukiwekwa kando,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Askofu Mkuu Anthony Muheria na Askofu Mkuu Martin Kivuva.
Maaskofu hao waliwataka wanasiasa kuzingatia utawala hadi kipindi rasmi cha kampeni za uchaguzi ujao kitakapotangazwa.
“Msisimko unaotokana na mikutano ya kisiasa huleta furaha ghushi ambayo huficha mijadala mikubwa ya sera, na kupandisha joto la kisiasa,” iliongeza taarifa hiyo.
Kanisa lilionya dhidi ya ukabila, likisema kuwa kwa muda mrefu umekuwa ukitumika kama zana ya kisiasa ya kuzua mgawanyiko. Waliwataka Wakenya kukataa siasa za ukabila na kuzingatia umoja wa kitaifa.
Maaskofu hao pia walizua hofu kutokana na kuongezeka kwa visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela, wakisema vinadhoofisha utakatifu wa maisha.
“Uhai ni zawadi kutoka wa Mungu, na ni wajibu wetu mtakatifu kuulinda. Hakuna mtu anayepaswa kudhulumiwa au kunyimwa utu wake. Tunazitaka mamlaka kuchukua hatua madhubuti kukomesha vitendo hivi visivyo vya kibinadamu,” walisema.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini yamekariri wasiwasi sawa na wa maaskofu hao, yakiitaka serikali kuwajibisha vyombo vya usalama kwa kuwateka na kuwazuilia watu kinyume cha sheria na kutoweka kwa baadhi ya waathiriwa.
Maaskofu hao pia walishutumu ufisadi uliokithiri, na kukosoa utumizi mbaya unaoendelea wa pesa za umma.
Waliitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi kuzidisha vita dhidi ya ufisadi, wakisema kuwa ufisadi unaendelea kuwanyima Wakenya huduma muhimu.
“Licha ya ahadi za mageuzi, ufisadi umesalia kukita mizizi. Tunatamani Kenya ambayo ufisadi hauna nafasi, na ambapo huduma zinatolewa bila hongo,” iliongeza taarifa hiyo.
Maaskofu hao pia waliisuta serikali ya Rais William Ruto kwa kukosa kushughulikia mzozo unaoendelea katika sekta ya afya, wakisema hospitali nyingi za kidini zinatatizika kutokana na kucheleweshwa kwa malipo.
“Hospitali zetu zinazohudumia watu walio hatarini zaidi, zimekwama huku serikali ikishindwa kurejesha fedha zinazodai tangu 2020. Zaidi ya Sh2.5 bilioni bado hazijalipwa, hivyo basi kuwa vigumu kuendelea kutoa huduma muhimu,” walisema.
Pia walitilia shaka mabadiliko ya haraka katika Hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF) bila mfumo ulio wazi, wakionya kuwa hatua hiyo imetatiza huduma za afya kwa Wakenya wengi.
Kuhusu uchumi, maaskofu hao walitaka hatua za haraka za kupunguza gharama ya maisha, wakitaja kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama vile chakula, umeme na usafiri.
Waliitaka serikali kufanya mazungumzo ya uwazi na wadau ili kupata suluhu endelevu.