Ichungwah alivyotolewa jasho akitetea utawala wa Ruto
KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah mnamo Alhamisi 27 alitolewa jasho akitetea utawala wa Rais William Ruto unaotuhumiwa kwa mauaji, utekaji nyara na ufisadi huku akidokeza kwamba Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ‘anakaribia kutimuliwa’.
Bw Ichung’wah alimshutumu Bw Muturi kwa kuendeleza siasa na suala la utekaji nyara na kueneza uwongo akilenga kuondoka serikalini.
Katika miezi ya hivi majuzi, Bw Muturi amekuwa akikashifu utawala wa Ruto hasa kuhusu utekaji nyara, akidai kuwa mwaka wa 2024 mwanawe alizuiliwa na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa usalama wa serikali wakati wa maandamano ya Gen Z na kuachiliwa tu rais alipompigia simu Mkurugenzi wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi Noordin Haji.
“Kuhusu malalamishi ya Muturi kwamba mwanawe alikuwa mwathiriwa wa utekaji nyara na aliachiliwa tu wakati yeye (Muturi) alipotafuta usaidizi wa rais, nilisoma tu kwenye vyombo vya habari na kumsikia akizungumza, lakini bado hatujasikia maelezo kutoka upande wa rais,” Bw Ichung’wah alisema katika kipindi cha runinga ya Al Jazeera, Head to Head, kilichoandaliwa na Mehdi Hasan.
Aliendelea: “Bw Muturi ni mwanasiasa na ana uhusiano mzuri na bosi wake Rais Ruto. Kuna sababu zilizomfanya aondolewe kama Mwanasheria Mkuu wakati wa maandamano ya Gen-Z (mnamo 2024) na pengine kuna sababu kwamba yuko njiani kuondoka serikalini.
Mbunge huyo wa Kikuyu na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa alisema waziri huyo ‘anaendeleza siasa’ na suala hilo na ‘yeye (Bw Muturi) anajua kwa hakika yuko njiani kuondoka baraza la mawaziri”.
Bw Ichung’wah, ambaye anajulikana kwa kukataa mahojiano na vyombo vya habari vya ndani hasa baada ya kupata kiti cha Kiongozi wa Wengi, alisafiri hadi London kwa mahojiano na Al Jazeera ili kukabiliana na maswali ambayo alitatizika kujibu.
Waliohudhuria ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Amnesty International-Kenya Bw Irungu Houghton, ambaye alisisitiza kuwa nchi hii ni kitovu cha utekaji nyara na mauaji ya watu wanaopinga serikali, akisema kwamba takwimu zilizorekodiwa zinazidi zile ambazo zimeripotiwa katika mapambano baada ya uhuru.
Bw Houghton alisema ni jukumu la Rais kuagiza utekaji nyara ukomeshwe na kuwawajibisha wale wote wanaohusika.
Katika mahojiano hayo, Bw Ichung’wah alikiri kuwa utawala wa Ruto haujaridhisha lakini akakanusha madai ya mtangazaji huyo wa Al Jazeera kwamba ‘umepoteza umaarufu kabisa’.
Ilianza pale mwandalizi alipodai kuwa rais Ruto alitoa ahadi 281 katika manifesto ya Kenya Kwanza mwaka wa 2022 lakini ametimiza takriban 14 kati ya hizo, akitaja ripoti ya Mzalendo Trust, shirika lisiloegemea upande wowote linalofuatilia shughuli za bunge.
“Ni kweli kuna maoni kwamba Rais Ruto hapendwi…si jambo lisilo la kawaida kwa utawala ulioingia mamlakani miaka miwili iliyopita ukiwa na ahadi nyingi lakini hilo litabadilika kadiri wakati unaposonga. Tulipata uchumi uliodorora,” Bw Ichung’wah alisema.
Aliongeza kuwa “utekelezaji wa manifesto ni ukurasa kwa ukurasa, sura kwa sura, sentensi kwa sentensi…inafanyika. Ni miaka miwili tu, siwezi kutoa jibu la uhakika kuhusu ahadi mahususi zilizotimizwa”.
Bw Ichung’wah pia aliulizwa ni kwa nini serikali bado haijaidhinisha mkataba kuhusu watu kutoweka licha ya utekaji nyara, mauaji ya kiholela na mateso nje ya mfumo wa sheria.
“Tuliahidi ndiyo, lakini je, kuna muda uliowekwa?’ Ichung’wah aliuliza.
Rais pia alikuwa ameahidi kuunda tume ya uchunguzi kuhusu mapendeleo na kutekwa kwa serikali ndani ya siku 30 baada ya kuingia mamlakani, swali ambalo lilimfanya Bw Ichung’wah kuwa na wakati mgumu kumtetea.
Hata hivyo, akilalamika kuwa hapewi nafasi ya kujibu maswali, alisema “hakuna jinsi mtu anaweza kuhukumu utekelezaji wa miradi ndani ya miaka miwili kuhusu kile ambacho kingetekelezwa katika miaka mitano”.
Alisema Serikali imetekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kutoa ruzuku ya uzalishaji badala ya matumizi kwa kutoa mbolea ya bei nafuu na hivyo kupunguza gharama ya maisha.
Prof Awino Okech wa Chuo Kikuu cha London, ambaye alikuwa mwanajopo, alisema: “Wakenya kila mahali wameonyesha kutokuwa na imani na serikali yao…hakika utawala huu umepungiwa na uaminifu.”