Hospitali za kibinafsi zalalamikia usiri wa mfumo wa malipo wa SHA
HOSPITALI za kibinafsi zimeitisha maelezo kamili kuhusu mfumo mpya wa malipo chini ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) zikionya ukosefu wa uwazi huenda ukazifanya zikose imani nao.
Wahudumu wa afya chini ya Muungano wa Hospitali za Kibinafsi Mashambani na Mijini (RUPHA), wameitaka SHA kuwapa maelezo kuhusu mfumo maalum unaopima mzigo wa maradhi na unaotumika kuamua ni kiasi kipi cha hela daktari au hospitali anapaswa kuwatoza au kuwalipisha wagonjwa wasio wa kulazwa kwa huduma fulani.
Kukosa kufanya hivyo, walisema, kutaruhusu bima hiyo ya kitaifa kusheheni mamlaka yasiyodhibitiwa na mabadiliko kiholela ya bei, hali inayoweza kuathiri pakubwa hospitali na kuifanya vigumu kupanga bajeti kuhusu gharama za huduma.
“Kama mfumo huo hautawekwa wazi, unaweza ukabadilishwa wakati wowote kumaanisha malipo huenda yakabadilikabadilika kiholela. Watoaji huduma huenda wakalazimika kupatia kipaumbele kutibu hali zenye mapato ya juu na kutelekeza nyingine,” alionya Mwenyekiti wa RUPHA, Dkt Brian Lishenga.
Mfumo unaoangaziwa ambao SHA imeweka siri unahusu tu matibabu ya wagonjwa wasio wa kulazwa chini ya Huduma ya Afya ya Msingi lakini haujumuishi huduma za wagonjwa waliolazwa na maradhi sugu kama vile saratani na ugonjwa wa figo.
“Hii ina maana, kwa mfano, nikimtibu mgonjwa malaria na nimonia kwenye kitengo cha mgonjwa asiye wa kulazwa, kisha mawasilisho ya malipo yatumwe kwenye mfumo, sitalipwa fedha ninazodai, SHA itatumia mfumo wake kuamua kiasi watakachonilipa,” anafafanua Dkt Lishenga.
Anahoji kuna uwezekano mkubwa kwa wanaotoa huduma za afya kuanza kupendelea kutibu hali fulani kwa sababu ya kujaribu kukadiria malipo watakayopokea.“Huduma ya kutunza itakuwa ghali kwa sababu wagonjwa walio na hali zisizowapa watoaji huduma mapato makubwa watatibiwa wapi? alihoji.
Anaeleza: “Chukulia kwa mfano nimonia itanipa fedha zaidi kuliko malaria, basi kuna uwezekano mkubwa nitazingatia zaidi visa vya nimonia kwa sababu malaria hainipi mapato. Hii itazorotesha ubora wa huduma za afya wanazopokea Wakenya. Nashangaa ni kwa nini serikali iliamua kufuata mkondo huo kwenye mfumo wa huduma ya afya.”
Hata hivyo, Katibu wa Wizara ya Huduma za Matibabu, Harry Kimtai amesema hakuna sababu ya kuhofia na hakuna usiri.
“Si eti tunaweka hili kuwa siri. Hatutaki kurejea kwa kilichotokea na NHIF ambapo hospitali zinawasilisha madai ya malipo kwa huduma ambazo hazikutolewa na kuvuna kutoka kwa mamlaka. Tunajihadhari tu, hii haihusu kuwaadhibu wamiliki wa hospitali,” alisema Bw Kimtai.
Alisema kila ugonjwa ana kipimo chake na kitasawazishwa katika vituo vyote.“Hakuna kituo kitakachopata malipo ya kiwango cha juu zaidi kushinda kingine kwa kutibu ugonjwa. Tufanye kazi kwa kutumia hii kwa maslahi ya Wakenya. Tunajishughulisha zaidi kuhusu tunachopata badala ya kutilia maanani huduma,” alisema.