Unadharau na kutesa mkeo? zinduka kaka
KUNA siri ambayo wanaume wanaodharau na kutesa wake wao hawajui.
Siri hii ni kuwa wanawake wanachangia pakubwa katika ufanisi wa waume wao. Wanaume wengi waliofaulu na kuwa na mali na familia thabiti huwa wanahusisha ufanisi wao na mchango wa wake wao.Mwanamume asiyeheshimu mkewe ni bure.
Hawa ni wale wanaume waliotekwa na kuganda katika itikadi zilizopitwa na wakati ambazo wanawake walichukuliwa kama vyombo vya kutumiwa na wanaume na kuwazalia watoto.
“Inasikitisha kwamba hata katika karne hii, wapo wanaume katika baadhi ya jamii wanaochukulia wanawake kama viumbe duni na kuwataka kupiga magoti mbele yao kuwatii hata wakati haki zao za kimsingi zinakiukwa,” asema mshauri wa wanandoa Janet Mbii.
Wanaume kama hao, asema, wanafaa kupatiwa mafunzo watambue kuwa mwanamke anapoheshimiwa, hurudisha heshima hiyo maradufu kwa mumewe na anapodharauliwa, huwa analipiza kwa dharau pia.
“Mume anayewezesha mkewe kwa hali yoyote ile, huwa anavuna matunda ya maisha yenye amani, mapenzi tele na familia thabiti. Kazi ya mwanamke si kupikia mumewe na kumtandikia kitanda kisha ampashe joto. Mwanamke ana haki ya kuheshimiwa na kuruhusiwa kutoa maoni yake katika ndoa sio kuwa mtumwa wa mumewe na jamii jinsi baadhi ya watu wanavyowachukulia,” asema Mbii.
Katika ulimwengu wa kisasa ambao wanawake wanapata elimu sawa na wanaume, maoni yao hayafai kuchukuliwa kuwa duni.“Baadhi ya wanaume huwa wanakosea kwa kuendesha udikteta katika ndoa kwa kutawaliwa na imani potovu za kijamii na kidini kuwa wake wao wanapaswa kukubali kila wanachotaka wafanye na hawafai kutoa sauti mbele yao,” anasema.
Anaongeza, “Huu ni ukandamizaji unaonyima mwanamume nguzo muhimu sio tu ya ufanisi wake bali pia furaha yake. Ukweli mchungu ni kwamba mke wa mtu ni wake peke yake na sio wa jamii baadhi ya wanaume wanavyosisitiza kama kisingizio cha kuwadharau wake wao,” aeleza Patrick Siacho, mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya ndoa.
Anasema enzi za wanaume kutisha wanawake kwa kusingizia desturi za jamii zimepitwa na wakati huku wanawake wakiendelea kusoma na kufunguka macho.
“Kufunguka macho kwa wanawake, kunafuta dhana kwamba ni viumbe wa kufungwa nyumbani, wasio na uhuru wao wa kujumuika na marafiki kwa shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Mwanamume asiyemhusisha mkewe katika mipango yake huwa amepoteza mwelekeo kabisa na kuwa kama kipofu,” asema Siacho.