Tuacheni tuomboleze kwa amani, familia ya Chebukati yawasihi Wakenya
FAMILIA ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wellington Wafula Chebukati imewasihi Wakenya kuiruhusu kumpa mpendwa wao mazishi ya heshima.
Familia imesinywa na kile inachotaja kama kuharibiwa jina kwa mpendwa wao na baadhi ya Wakenya, haswa kwenye mitandao ya kijamii wakisema ni mtu asiye na hatia ambaye alikuwa na utu na uadilifu wa hali ya juu.
Bw Chebukati ambaye alimaliza muda wake wa miaka sita usukani mwa IEBC mnamo Januari 17, 2023, alifariki akiwa na umri wa miaka 63.
Lakini familia yake sasa inalalamika kwamba maoni ya Wakenya kwenye mitandao ya kijamii kuhusu jamaa yao ya kumpaka tope rekodi yake katika utumishi wa umma.
Kulingana na familia, tatizo la afya la marehemu Chebukati lilianza punde tu alipomaliza kusimamia Uchaguzi Mkuu wa 2022 mnamo Novemba alipoanza kulalamika kuhusu maumivu katika jicho moja.
Madaktari wake baadaye walithibitisha kwamba alikuwa akiugua uvimbe wa ubongo.
“Alianza kulalamika maumivu kwenye jicho na baadaye alisafiri hadi Ujerumani mara mbili kwa upasuaji. Tangu wakati huo, afya yake haikuimarika na alikuwa akiingia na kutoka hospitalini hadi kifo chake mwishoni mwa mwezi uliopita,” kakake Daniel alisema kwenye mkutano wa familia.
Wakizungumza nyumbani kwao Kapomboi, eneo bunge la Kwanza, familia ilisema imeathirika pakubwa na kile ilichotaja kama kukashifiwa kwa tabia ya marehemu kwenye mitandao ya kijamii.
Ikiongozwa na babake John Wafula Chebukati, mamake, Joina Nekesa, na kakake Daniel Chebukati, familia hiyo imewataka Wakenya kuwaruhusu kuomboleza jamaa yao na kumzika kwa amani wikendi ijayo.
“Inauma kwetu kama familia kwamba tumempoteza, na ningependa kuwaambia Wakenya kwamba mtu wanayemsulubisha hana hatia, na wanamsulubisha kwa dhambi ambazo hakuwahi kufanya. Huyu ni mtu tunayemjua vyema na alikuwa msafi kama theluji,” kaka yake alisema.
Familia hiyo inajitayarisha kuupokea mwili wake Ijumaa ijayo nyumbani kwao Kapomboi kwa maombi kabla ya kuzikwa nyumbani kwake Sabata, eneo bunge la Kiminini mnamo Machi 8.
Familia ilisema kuwa licha ya kifo chake, wana kumbukumbu nzuri za jamaa yao kama mtu mnyenyekevu ambaye hakupenda mambo mabaya katika kazi yake.
“Watu wanasema mambo mengi sana kuhusu mtoto wetu. Ni baada ya kufa tu ndipo unapowajua adui na marafiki zako. Imekuwa uchungu sana kwetu kama familia kumpoteza mwana wetu,” babake alisema.