Habari

Serikali yaomba utulivu ikichunguza ugonjwa usiojulikana Kisii

Na GEORGE MUNENE March 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

UGONJWA wa ajabu ambao haujabainika kufikia sasa umeripotiwa katika Kaunti ya Kisii huku serikali ikisema inafuatilia kudhibiti mlipuko.

Walioathiriwa wanaonyesha dalili za joto jingi, kuendesha na kisunzi na sasa maafisa wa afya wanakusanya sampuli za kufanyia uchunguzi.

“Kuna ugonjwa wa ajabu Kisii. Wale wanaoenda hospitalini wanateta kuwa wanaendesha na kuwa na joto sana. Tumetuma kikosi cha madaktari Kisii ili wachukue sampuli kuwezesha utambuzi wa ugonjwa huo,” akasema Katibu wa Idara ya Afya ya Umma katika Wizara ya Afya, Mary Muthoni akiwa Mwea, Kaunti ya Kirinyaga mnamo Jumapili.

Bi Muthoni amerai wananchi wawe na utulivu akisema hali hiyo inadhibitiwa.

“Tutaarifu taifa kuhusu hatua tuliyopiga tunaposonga mbele,” akaeleza.

Kulingana na Bi Muthoni, serikali ya kitaifa inashirikiana kwa ukaribu na ile ya Kaunti ya Kisii kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.

“Jukumu la afya limegatuliwa ila panapoibuka mlipuko wa ugonjwa, tunafanya kazi kwa umoja ili kuokoa maisha,” akasema.

Serikali imeahidi kuweka mikakati ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo pindi tu itakapobainika huku ikitaka Wakenya wasiwe na hofu kwa kuwa inashughulikia hali kwa makini.

Kadhalika, Bi Muthoni amesema serikali inapambana na ugonjwa wa homa ya nyani ambao umeripotiwa nchini.

“Pia tuna mlipuko wa ugonjwa wa Monkeypox na Wakenya wanapaswa kuwa waangalifu wasiambukizwe,” aliarifu.

Alionya Wakenya waepuke kukaribiana na watu wanaougua ugonjwa huo ili wawe salama.

“Ni muhimu kwa Wakenya kuzingatia kanuni za usafi ili kuepuka kuambukizwa homa hii, ugonjwa ambao uliingia nchini kutoka nchi jirani,” aliongeza.

Kuhusu Hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF), Bi Muthoni aliwaomba Wakenya kupuuza taarifa alizoziita propaganda akiwarai kujisajili.

Japo bima hii inapingwa, Katibu Muthoni amesema iko sawa, “SHIF ina matatizo machache ambayo yanashughulikiwa lakini inafanya kazi, Wakenya wanapaswa kuikumbatia,” alisema.