Jamvi La Siasa

Gachagua aonywa kwa kutishia Ruto akimwambia ‘akae Nairobi’

Na BENSON MATHEKA March 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imetoa onyo kali kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa matamshi yake ambayo inasema ni ya kiholela.

Tume hiyo Jumatatu ilisema imempa Bw Gachagua notisi ya kusitisha matamshi yake ambayo inahisi yanavuka mipaka.

“Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano imetoa notisi kwa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, ikimtaka aache kutoa matamshi ambayo yanakiuka Sheria ya NCIC Nambari 12 ya 2008,” NCIC ilisema katika taarifa.

Tume hiyo yasema kwamba, mara kwa mara, Gachagua amekuwa akikiuka Sheria ya NCIC, ambayo inaharamisha ubaguzi wa kikabila, rangi na kidini.

Kifungu cha 13 cha sheria hiyo kinaharamisha matamshi ya chuki na hivyo kufanya kuwa kosa kwa mtu yeyote, haswa viongozi wa kisiasa, kutumia maneno ya vitisho, matusi na uchochezi dhidi ya mtu, kikundi au jamii yoyote.

Katika taarifa yake, NCIC hasa ilinukuu moja ya kauli za hivi punde za Gachagua kuhusiana na Jaji Mkuu Martha Koome, ambapo aliapa kuongoza maandamano iwapo ataondolewa ofisini.

Akizungumza katika kanisa la AIPCA St Joseph KK Garu, Wadi ya Antubetwe-Kiongo, Igembe Kaskazini katika Kaunti ya Meru mnamo Februari 23, Bw Gachagua, alimkosoa vikali Rais William Ruto ambaye alimshutumu kwa kujaribu kufifisha ushawishi wa kisiasa eneo la Mlima Kenya.

“Tunajua anapanga kumuondoa Koome ofisini. Sasa amezidi. Unaondoaje uongozi wa jamii nzima iliyokufanya rais?” Bw Gachagua aliuliza.

Kulingana na NCIC, kauli hii ya Gachagua ya kuhimiza jamii kupinga kutimuliwa kwa Koome, ni ya uchochezi.

“Madai yako kwamba kuna njama iliyobuniwa na Rais ya kumwondoa Jaji Mkuu ofisini kwa sababu ya kabila lake ni ya kupotosha na yanalenga kukuza ukabila na kuna uwezekano wa kuibua hisia za uhasama miongoni mwa Wakenya na hivyo basi kuhujumu umoja na amani,” NCIC ilionya.

Tume hiyo pia ilimkashifu Gachagua kwa kutuma ujumbe wa vitisho alipomwonya Rais Ruto dhidi ya kuenda Meru ikiwa Koome atapoteza kiti chake.

Katika matamshi yake Februari, Gachagua alionya viongozi kwamba wataondolewa afisini katika uchaguzi mkuu ujao kupitia chama chake cha kisiasa ambacho anapanga kukizindua Mei mwaka huu.

Jana, mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga alisema japo kiongozi wa chama hicho Raila Odinga anasikiliza maoni kabla ya kutangaza mwelekeo wa kisiasa baada ya kushindwa kutwaa uenyekiti wa Muungano wa Afrika (AUC), matamshi ya Bw Gachagua yanatia hofu.

Bi Wanga alisema japo Bw Odinga hapuuzi mwaliko wa Bw Gachagua kuungana naye na viongozi wengine wa upinzani, ODM ina wasiwasi kuhusu matamshi ya Gachagua.

“Kuna wasiwasi na dalili za hatari. Kwa mfano, mtu akisema ‘sisi ni wa eneo hili na eneo hili litafagia viti, kwa mfano mahali fulani kama Nairobi’ basi tunaogopa sana kwa sababu ODM daima limekuwa vuguvugu la kitaifa,” Wanga alisema.

Bw Gachagua, amemwalika Bw Odinga ambaye amechangamkia Rais Ruto kuungana naye na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa, na kiongozi wa People’s Liberation Party (zamani NARC-Kenya) kuunda muungano wenye nguvu wa kisiasa kwa lengo la kumwondoa madarakani Rais William Ruto.