Dondoo

Ashangaza waumini kuwachezea wimbo wa mapangareh kanisani!

Na SAMUEL MUIGAI March 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAUMINI katika kanisa la Gachie mjini Kiambu walipigwa na butwaa kwenye ibada wakati mgeni aliyealikwa kuwasalimia aliwachezea wimbo wa kizazi kipya wa mapangareh.

Kanisa hilo halina waumini wengi na hivyo, kama kawaida, pasta alipoona uso mgeni aliomba wote waliokuwa wamefika hapo kwa mara ya kwanza wasimame ili wakaribishwe rasmi.

Ni polo pekee aliyeinua mkono. Pasta akamuomba afike mbele ya waumini awasalimu.

Mgeni hakusita, alisonga mbele na kujitambulisha kama msanii chipukizi na kisha akaanza kusakata densi ya mapangare hata kabla ataje jina lake.

Ilibidi pasta anyanyuke aende kumkatiza na alipomkaribia ndipo aligundua jamaa alikuwa mlevi.