Mwanavishale Wachiuri arejea nyumbani kama mfalme baada ya kufana Uingereza
NYOTA wa kurusha vishale Peter Wachiuri aliondoka nchini Februari 22 usiku kama mtu wa kawaida tu, lakini alirejea nyumbani Jumatatu akiwa shujaa aliyesisimua mashabiki mitandaoni.
Hii ni baada yake kuonyesha talanta ya hali ya juu kwenye mashindano ya kimataifa ya MODUS Super Series yaliyoandaliwa mjini Portsmouth, Uingereza, kuanzia Februari 24 hadi Machi 1, 2025.
Dereva huyo wa teksi alicheza michuano 29 na kumaliza nambari mbili kati ya washiriki 12 wenye uzoefu mkubwa.
Wachiuri, 38, alipoteza katika fainali dhidi ya Scott Campbell kutoka Scotland kwa mikondo 4-1 hapo Jumapili. Alijizolea tuzo isiyopungua Sh400,000 (Pauni 2,500). Mshindi alipokea zawadi maradufu.

Wachiuri alisisimua mashabiki na mchezo wake na pia anavyosherehekea kila ushindi.
Kwa kufika fainali ya ligi hiyo ya kifahari ya MODUS Super Series, Wachiuri alijikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la wachezaji wawili wawili la MODUS (MODUS Doubles World Cup) litakalofanyika mjini Portsmouth mwezi Aprili.
Wachiuri anatoka katika timu ya Buffalos inayoshiriki Ligi ya Vishale ya Afrika (ADS). Alifungulia Mkenya mwingine mmoja kuenda naye kwenye dimba la dunia.
MODUS Super Series ni mashindano yanayofanyika kila wiki yakikutanisha wachezaji 12 kutoka Jumatatu hadi Ijumaa halafu fainali ni Jumamosi usiku.
Wachiuri alilemea Muingereza Colin Osbourne 4-3 katika nusu-fainali naye Campbell alipepeta Muingereza Kevin Burness 4-0 katika awamu hiyo.
Kampuni ya Sirua Darts Group ilisema kuwa Wachiuri aliwakilisha zoni ya Mashariki na Kaskazini barani Afrika katika mashindano hayo.