Mlemavu msomi aliyetaka kuwa mhandisi sasa anashikilia rekodi ya javelin Afrika
MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika ya kurusha mkuki kwa watu walio na ulemavu wa macho (F12/13) Sheila Wanyonyi amefichua kwamba alikuwa na ndoto ya kuwa mhandisi akiwa mtu mzima, lakini haikuwezekana.
Licha ya kuzaliwa na ulemavu wa kukosa kuona nyakati kuna giza ama mwangaza mdogo, Wanyonyi amejaa matumaini kuwa anaweza kufikia na hata kufuta rekodi ya dunia iwapo atapata usaidizi muhimu.
Wanyonyi alizaliwa katika eneobunge la Bumula, Kaunti ya Bungoma, mwaka 1998 na kusoma katika shule za vipofu za St Francis School for the Blind (Kapenguria, Pokot Magharibi) na Thika High School for the Blind (Kiambu).

Alifuzu na digrii katika Masuala ya Jinsia na Maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta (Nairobi) mwaka 2023.
Nilipokuwa mdogo, ndoto yangu ilikuwa kuwa mhandisi. Hata hivyo, nilipogundua watu walio na ulemavu hawawezi kufanya masomo ya sayansi (fizikia na kemia) bali “Adoptive Biology” nilihisi kuchanganyikiwa
Wanyonyi hakujua afanye nini baada ya kufahamu hilo.
“Nilijaribu kubadilisha kozi yangu nilipojiunga na kidato cha kwanza 2015 katika shule ya Thika School for the Blind. Nikiwa huko tulialikwa kwa mazungumzo kama wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuulizwa taaluma ambayo tungependa kufanya,” anatanguliza katika mahojiano.
“Hata hivyo, niliposimama na kusema nataka kuwa mhandisi nilififia moyo kuambiwa mtu asiyeona hawezi kufanya kozi hiyo. Hapo ndipo nilijua sisi wenye tatizo hilo hatuwezi kufanya kozi za kemia na fizikia bali Adoptive Biology, ambayo kwangu nilihisi haiwezi kunisaidia sana,” alieleza.
Vizingiti kote kote
Wanyonyi alipiga moyo konde na kudhani kwa sababu anapenda hisabati angegeukia uhasibu. “Nilivunjwa moyo tena kwamba siwezi fanya kozi hiyo. Kozi pekee nilishauriwa nichague ilikuwa elimu ama sheria. Lakini sikutaka taaluma hizo, wala sikujiona nikisimama mbele ya wanafunzi kufundisha,” asema.
Hali ilikuwa ngumu kwake kwa sababu pia alifanya kozi ya mhudumu wa kike katika ndege, ambayo vile vile hakufanikiwa kupata kazi.
“Niliamua sasa kuchukua kozi yoyote itakayokubalika. Ulemavu wangu ulifanya niwe hapo tu bila ya chaguo lililonipendeza. Niliendelea na mosomo lakini bila motisha,” anaeleza.

Wanyonyi alidhani kuwa anaweza kupata kazi kutokana na kozi za sayansi ya nyumbani ama hisabati, lakini “nikapata kuwa somo ambalo lingenisaidia ni sayansi za jamii ukizingatia changamoto zilizopo.”
“Tuliambiwa kuwa mtu asiyeona anaweza kufanya tu ualimu ama sheria. Nilipokamilisha masomo ya shule ya upili niliitwa Chuo Kikuu cha Pan African na pia kile cha Kikatoliki (CUEA). Vyuo hivi vilitaka nifanye saikolojia ya kutoa ushauri nasaha. Hata hivyo, havikuwa na vifaa vya walemavu ndipo nikaamua kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) ambako sasa ninasomea kozi ya masuala ya jinsia. Ilibidi nipende kozi hiyo kwani ndiyo niliangukia,” akasema Wanyonyi aliyefuzu na digrii ya Masuala ya Jinsia na Maendeleo kutoka KU mwaka 2023.
Akiwa Kenyatta, Wanyonyi alipata kufahamu kuhusu mchezo wa kurusha mkuki. Alifundishwa mchezo huo na Dkt Samwel Litaba ambaye ni kocha wa riadha katika chuo hicho.
Alinifundisha jinsi ya kukamata mkuki. Hapo ndipo safari yangu ya kurusha mkuki ilianzia
Rekodi zatamba
Kabla kuingilia urushaji mkuki Wanyonyi alidhania ni mchezo hatari. Hata hivyo, tangu akite humo mchezo huo umemfanya apande ndege kuenda Ghana, Nigeria, Tunisia, Japan, Ufaransa na Milki za Kiarabu (UAE) kushiriki mashindano.
Katika ziara yake majuzi, Wanyonyi alishiriki mashindano ya Dubai 2025 World Para Athletics Grand Prix kule UAE.
Alirusha mkuki umbali wa mita 30.40, 35.03m, 27.55m, 25.99m, 29.44m na 24.67m katika mitupo yake sita ya kitengo cha F12. Matokeo hayo yalimwezesha kutwaa taji kwa rekodi mpya ya bara Afrika ya 35.03m.
Mchina Yuping Zhao anashikilia rekodi ya dunia kitengo hicho baada ya kurusha mkuki 47.06m alipojishindia dhahabu kwenye Olimpiki za Paris 2024.
Lengo langu sasa ni kufikia rekodi ya dunia ikiwezekana kabla Michezo ya Olimpiki ya Walemavu mwaka 2028
Wanyonyi pia analenga kueneza injili ya Olimpiki mashinani.
“Walemavu wengi hawana habari kuhusu Olimpiki ya Walemavu. Nataka niwafikie ili tuweze kuimarisha idadi ya wachezaji na pia ushindani,” alihoji Wanyonyi.

Alifurahi sana kupata rekodi ya Afrika mjini Dubai mwezi Februari. “Sikuamini macho yangu kwa sababu nilikuwa napata mirusho ya mita 30, 31, 32, 28, lakini nikaandikisha 35,” asema.
Anaamini anaweza kuimarisha rekodi hiyo yake na hata kuweka mpya ya dunia akipata usaidizi mzuri wa vifaa, kifedha na maandalizi
Ilipothibitishwa kuwa rekodi ya Afrika ilinipa motisha tele. Ilinifanya nihisi kwamba naweza kufikia rekodi ya dunia
Shujaa wake katika urushaji mkuki ni Andreas Thorkildsen, 42, wa Norway anayejivunia kushinda mataji ya Olimpiki mwaka 2004 na 2008, dunia (2009) na bara Ulaya (2006 na 2010).
“Kinachonipendeza kumhusu ni ustadi wake na moyo wa kujituma. Nilisoma kumhusu akiwa bingwa, kufifia na hatimaye kurejea tena kwa kishindo. Sifa hizo ni za kipekee na zinanitia moyo kila siku kama mwanamichezo. Mbinu zake za kurusha mkuki pia bado zinatumiwa na makocha,” akaeleza.
Goalball
Mbali na kurusha mkuki, Wanyonyi pia ameshiriki mpira wa mikono almaarufu goalball. Hivi majuzi pia alijitosa katika uendeshaji baiskeli.
Wanyonyi amejifunza mengi kupitia michezo. “Nimepata nidhamu. Ukiwa mwanamichezo lazima pia ufahamu mambo ya lishe usije ukapigwa marufuku kwa kutumia bidhaa ambazo zina kemikali za kusisimua misuli. Si haki kutumia njia haramu kushinda wenzako. Michezo pia imenifundisha kuepuka maovu pamoja na kuweka malengo na kutia bidii hadi niyatimize,” asema.