Mizozo, ukosefu wa uwazi katika bajeti na siasa zinavyotishia Ushanga Kenya
MIGOGORO, bajeti isiyo wazi na kuingiliwa na wanasiasa zinasemekana kubomoa mafanikio yaliyochukua miaka kadhaa katika Mpango wa mamilioni wa Ushanga Kenya na kuweka hatarini Vyama vya Ushirika 187 vya wanawake nchini kote.
Mpango wa Ushanga Kenya ulianza Oktoba 2021, miaka mitano baada ya kuzinduliwa, kabla haujabadilika na kuwa shirika la kibiashara mwaka wa 2023 chini ya Wizara ya Utalii, Wanyamapori na Urithi ili kuhakikisha kuwa shanga zinazoundwa na wanawake wa Kenya zinalindwa ndani na nje ya nchi. Pia, shirika hili lilipewa jukumu la kukuza urithi wa kitamaduni na uwezeshaji wa wanawake kupitia ujasiriamali.
Hata hivyo, mizozo katika usimamizi wa shirika hilo kubwa la mashinani inaonekana kuwa mikubwa hadi kughadhabisha mamia ya wanawake katika ngazi ya mashinani hasa kutoka kaunti kame.
Katika mahojiano ya kipekee, Afisa Mkuu Mtendaji Bi Dorothy Mashipei alielezea hali ya huzuni ya shirika hilo iliyotokana na vita vya ubabe, bajeti isiyoeleweka na kuingiliwa kisiasa inayotishia biashara ya mamilioni.
Bi Mashipei ambaye amekuwa katika kilele cha mpango huo tangu kuanzishwa kwake alisema usimamizi duni umekumba mpango huo katika miaka mitatu iliyopita.
“Matatizo makubwa ya usimamizi yalianza wakati mpango huo ulipowaziwa chini ya afisi ya Naibu Rais wakati huo William Ruto ( sasa rais) katika muhula wa pili wa utawala wa Rais Kenyatta. Kulingiliwa na wanasiasa kulisababisha mgao wa awali kuondolewa na kuhamishwa kwingine. Kufikia sasa, hatuna afisa mkuu wa uhasibu. Afisa uhasibu yeyote anaweza kuelekeza fedha hizo kwenye shughuli nyingine,” alisema Bi Mashipei
Alilalamika kuhusu bajeti ambayo haijafichuliwa ya mpango huo akisema unatumia bajeti inayodhibitiwa kutoka mahali pengine na kuufanya kutumiwa na kundi la watu serikalini kuiba pesa.
“Licha ya kutengewa pesa kila mwaka na bunge, tumekuwa tukifanya kazi kwa bajeti isiyoeleweka. Hili ni suala ambalo nimelizungumza kwa mara nyingi na Mwenyekiti na Katibu wa Wizara. Binafsi sijui tuna kiasi gani. Kwa miaka miwili iliyopita hatujaweza kutengeneza bidhaa,” alisema kwa uchungu.
Afisa Mkuu Mtendaji alilalamikia mafunzo ya wanawake yanayotolewa kwa upendeleo na uwezeshaji unaoshawishiwa na wanasiasa kutimiza maslahi yao. Alidokeza kuwa angalau wanawake 100,000 kutoka vyama vya ushirika 187 katika kaunti 10 wamekuwa walengwa lakini wanasiasa wanavuruga mradi huo. Kaunti ya Kajiado inajivunia Vyama 92 vya Ushirika.
“Kutokana na ushawishi wa kisiasa, mafunzo na uwezeshaji siku hizi yanafanywa kwa njia ya upuuzi. Hauwezi kujua ni akina nani wanaolengwa na idadi yao. Uendelevu wa mpango huu umetikiswa hadi msingi,”aliongeza.
Alisikitika kuhusu kupunjwa kwa wanawake chini ya mpango huo akisema kuwa unapaswa kuweka mkazo zaidi katika biashara ya kijamii ili kumlinda mwanamke.
Hata hivyo, pamoja na matatizo haya, Bi Mashipei alisema mpango huo umeweza kupunguza mwanya katika masoko ya bidhaa za sanaa duniani na kuanzisha uhusiano wa soko na wanawake wanaotengeneza shanga vijijini.
“Tumeweza kuunganisha makumi ya wanawake na soko la kimataifa. Mpango huu umebadilisha maisha ya watu wa vijijini hasa kwa sasa wanawake wengi wanapoacha ufugaji kutokana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mashipei.
Aliongeza: “Inasikitisha sana, huu ni mradi ambao ulikuja na matumaini makubwa kwa jamii. Mradi huu pia ulikuwa katika manifesto ya Kwanza ya Kenya, ninahofia kuingiliwa kisiasa na ukosefu wa usimamizi kunaweza kuangamiza mradi huo katika miezi michache ijayo.

Bi Ummi Mohamed Bashir Katibu wa Utamaduni na Urithi akihutubia wanahabari katika kaunti ndogo ya Kajiado mnamo Machi 3 2025.Picha/ Stanley Ngotho
Hata hivyo, mnamo Jumatatu Machi 3, 2025, Katibu wa Utamaduni na Urithi Bi Ummi Mohamed Bashir alisema serikali inajitahidi kuwaondoa mabroka ambao walikuwa wakifyonza faida ya bidhaa za Shanga kutoka kwa wanawake wa mashinani.
Akiandamana na Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Kajiado Bi Leah Sainkaire katika hafla iliyosusiwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa mpango huo Bi Dorothy Mashipei, na kufichua mzozo katika shirika hilo, Katibu ambaye alizindua mafunzo ya siku tano ya Ushanga kwa angalau wanawake 100 kutoka kijiji cha Naretoi huko Kajiado, alikubali matatizo yanayoathiri mpango huo lakini akajiepusha na vita baridi kuhusu usimamizi.
“Hivi karibuni sana jukwaa la biashara dijitali la Serikali ya Kitaifa la Sanaa litazinduliwa. Hili ni soko la kimataifa ambalo lina lugha saba tofauti. Tunataka wanawake wauze bidhaa zao ndani na nje ya nchi,” alisema Bi Bashir.
Aliongeza: “Tunashirikiana na shirika la Posta Kenya Tutazindua bidhaa baada ya miezi kadhaa. Tuko katika ulimwengu wa kiufundi na kidijitali ambapo kila kitu kinauzwa mtandaoni. Mara tu jukwaa la Sanaa E-commerce litakapoanzishwa litasaidia wanawake wa Ushanga. Wakiwa na chama cha ushirika, wanaweza kuweka pesa mfukoni moja kwa moja na kuepuka mabroka,”
Hata hivyo, Katibu alisita kufichulia Taifa Leo ni kiasi gani kimetengwa na Wizara kwa Mpango wa Ushanga Kenya.
Mwakilishi wa Wanawake wa Kajiado Bi Leah Sankaire alisema mpango huo umetekwa nyara na wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiwapunguzia fedha wanawake wa vijijini na wasiojua kusoma na kuandika.