MAONI: Kenya itapataje sifa nzuri ilhali inasaliti mataifa mengine?
HIVI Kenya imewezaje kudumisha mwonekano wa taifa la kidemokrasia ilhali vitendo vyake rasmi vinahujumu mfumo huo wa kiutawala ndani na nje ya nchi?
Sirejelei serikali ya sasa bali sera ya jumla ya serikali zetu zote tangu tupate uhuru miaka zaidi ya 60 iliyopita. Inaweza kuelezewa kama sera ya kichokozi au kiusaliti.
Hatujawahi kutoa mafunzo yoyote ya kiutawala wala kuyaunga mkono mataifa yaliyopata uhuru baada yetu. Barani Afrika, kazi hiyo ilifanywa zaidi na Ghana, Zimbabwe, Zambia, Tanzania na hata Libya, enzi ya marehemu Rais Muammar Gaddafi.
Nimesalitika kujiuliza swali la chanzo cha sifa za Kenya baada ya kuwaona wanaharakati wa haki za binadamu wakiandamana jijini Nairobi kupinga mateso ya serikali ya Uganda dhidi ya kigogo wa Upinzani, Dkt Kiiza Besigye.
Hao ni raia wa Kenya, ambao wamejasiria kuandamana hadi kwenye lango la ubalozi wa Uganda, Nairobi, wakawazomea walinzi na kuilaani serikali ya dikteta Yoweri Kaguta Museveni.
Wameshinikiza na ubalozi huo ufungwe kwa kuwa haki za kibinadamu za Dkt Besigye, Mganda, zimevunjwa kwa kusingiziwa uhaini, akasusia chakula, afya yake ikadhoofika vibaya mno.
Kumbuka Dkt Besigye alitekwa nyara na polisi wa Kenya alipozuru Nairobi, wakamkabidhi kwa serikali ya Uganda. Kwa ufupi, Serikali ya Kenya haiwezi kujiondolea lawama za kuwa mwezeshaji wa watesi wa mwanasiasa huyo.
Wakati ambapo mateso dhidi ya Dkt Besigye yanaendelea, Serikali ya Kenya imewapa waasi wa Sudan jukwaa la kuundia na kutangazia serikali mbadala, huku anga ya Khartoum ikinuka baruti! Hiyo si hatua patanishi bali tenganishi.
Kwa muda wa mwaka mmoja na ushei ambapo vita kati ya Israel na Hamas vimeendelea, Kenya imeiunga mkono Israel hata wakati ambapo wanawake na watoto wa Palestina wamedhulumiwa haki zao.
Si siri kwamba Kenya inamuunga mkono Rais wa Rwanda, Paul Kagame, anayeendesha harakati za kijeshi ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako anaua na kufukuza watu makwao.
Ukifuata historia, unapata kuwa Kenya iliwapa hifadhi makaburu waliokuwa kwenye serikali ya kibaguzi ya Afrika kusini wakati ambapo mataifa mengine ya Afrika hayakutaka uhusiano wowote nao.
Huku Kenya ikiwapa hifadhi makaburu hao walioona raha kuwatesa raia weusi wa Afrika Kusini, mataifa mengine ya bara hili yalikuwa shughulini kutoa mafunzo ya kijeshi na kusafirisha silaha kinyemela ili kuiangusha serikali hiyo dhalimu.
Marehemu dikteta wa Somalia, Siad Barre, alipotimuliwa nchini mwake baada ya kuwakalia raia mguu wa kausha kwa miongo kadha, Kenya ilimpitisha mpakani, ikamleta Nairobi na kumtunza kama beberu aliyenuiwa kuchinjwa wakati wa sikukuu.
Mara nyingi tukiambiwa na kurejelewa kwenye uga wa siasa kuwa watu si wajinga. Nakubaliana na kauli hiyo, ila nitaongeza kuwa watu werevu hawapatikani Kenya pekee.
Hulka ya serikali zetu hiyo ya kufungamana na mashetani wakati ambapo raia wema wanahitaji msaada wetu inajulikana nje ya nchi, na labda ndiyo sababu tunadharauliwa na baadhi ya mataifa.
Hata hivyo, watu hao werevu wana uwezo wa kutofautisha kati ya tabia mbaya za serikali, na moyo wa upambanaji wa Wakenya wa kawaida, ndiposa wanaitamani demokrasia yetu.
Wanachotamani si utu wala ukarimu wa serikali zetu katika kuheshimu haki zetu za kidemokraisa, la hasha! Wanaheshimu ujasiri wa Wakenya wa kawaida kumwagika barabarani na kumshinikiza dikteta akubali siasa za vyama vingi.
Wanatuvulia kofia kwa kudai mabadiliko ya Katiba na kufuatilia ili kuhakikisha inatumika ilivyo, angaa mara kadha, na wanasiasa wakishupaa shingo na kupitisha maozaoza bungeni tunaanguka nao mpaka wanashuka na kughairi nia mbaya.
Haikosi moyo huu wa upambanaji umemshtua Rais Museveni mno baada ya kutuona tukiandamana kwa niaba ya Waganda ambao amekandamiza miaka yote hii. Anajua tunaweza kuandamana tukielekea Kampala kutoka Nairobi, kumsalimu eti.
Huo ni moyo ambao Wakenya wanapaswa kudumu nao milele, tukatae kubadilika kabisa hata serikali zetu zikiendelea kufanya maamuzi ya kuudhi.