Wilbaro, mikokoteni kuhitajika nambari za usajili mswada wa Robert Alai ukipita
WAENDESHAJI wilbaro na mikokoteni katika jiji kuu la Nairobi sasa watahitajika kuisajili na kuvaa mavazi maalum iwapo mswada mpya uliowasilishwa katika bunge la kaunti hiyo utapitishwa.
Mswada uliowasilishwa na Diwani wa Kileleshwa Robert Alai, unanuia kuanzisha sheria zinazohusu aina yote ya vyombo vya usafirishaji mbali na magari (NMT) katika jiji kuu nchini.
Wilbaro, baiskeli, mikokoteni ya kuvutwa kwa mikono, mikokoteni inayovutwa na wanyama, troli za kubebea mizigo na hata bajaji ni vyombo vya usafirishaji vinavyolengwa katika mswada huo.
Pendekezo kuu mojawapo ni kuanzishwa kwa nambari za usajili kwa NMT huku waendeshaji wakihitajika kuvalia makoti na nembo zinazoangaza katika juhudi za kuimarisha nidhamu.
Kila NMT, mswada unaeleza, Itahitajika kusajiliwa na kupatiwa nambari maalum ya usajili inayoangaza. Bw Alai alieleza bunge la kaunti Jumanne mswada huo mpya utaboresha usalama kwa watumiaji barabara na kupunguza msongamano wa trafiki Nairobi.
“Ongezeko la matumizi ya vyombo vya usafirishaji kando na magari limesababisha msongamano jijini ambapo mikokoteni inayobururwa kwa mikono na troli zikiongoza kwa kusababisha ajali kutokana na mapuuza na utovu wa nidhamu uliokithiri miongoni mwa watumiaji wake,” alisema Bw Alai.
“Waendeshaji wengi wa vyombo hivi, kwa sababu ni watumiaji barabara, hawana maarifa yanayohitajika kuhusu usalama barabaranu na bima ya kuwakinga ajali itokeapo.”
Vyombo vya usafirishaji kando na magari vinatambuliwa chini ya Sheria kuhusu Trafiki 1998 lakini waendeshaji magari hukabiliwa na wakati mgumu kufidiwa baada ya ajali kutokana na ukosefu wa sheria mwafaka za kuwadhibiti na kuwatambulisha waendeshaji husika.
Iwapo bunge la kaunti ya Nairobi litapitisha mswada huo, watoaji huduma watahitajika kupaiwa sera ya bima itakayoowahakikishia usalama watumiaji wengine barabarani.
Wahudumu wana muda wa miezi sita kutimiza agizo la bima ikiwa mswada huo utaidhinishwa.
NMT inajumuisha asilimia 45 ya usafirishaji unaofanyika Nairobi, kulingana na ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP).
Udadisi uliofanywa na Halmashauri ya Kusimamia Huduma Nairobi (NMS) 2020 ilibaini safari 2.27 milioni zinazofanyika kila siku jiji kuu ni za watumiaji MNT.
Aidha, ilibaini watumiaji NMT wanachangia jumla ya asilimia 66.3 ya vifo kutokana na ajali za barabarani Nairobi.
Kwa kubalia makoti yanayoangaza, kudumisha nidhamu barabarani na kuvalia nembo, Bw Alai alifafanua kwamba wahudumu wa NMT watawajibika na kuwa na mpangilio zaidi hivyo kupunguza visa vya ajali.