Uchaguzi 2027: Wanawake waogopa kiti cha Chebukati, sita pekee watuma maombi
WAKENYA waliotuma maombi ya kutaka kujaza nafasi za mwenyekiti na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) watajulikana Alhamisi Machi 6, 2025 huku ikibainika kuwa ni wanawake sita pekee wanataka kushindania wadhifa wa mwenyekiti.
Mwenyekiti wa Jopo la kuteua makamishna wapya wa tume hiyo Nelson Makanda Jumatano, Machi 5, 2025 alisema kuwa jumla ya watu 37 waliomba nafasi hiyo, watatu wakiwa watu wanaoishi na ulemavu (PLWD).
“Kulingana na maombi tuliyopokea na kuchumbua, wanaume 31 waliomba nafasi ya mwenyekiti, idadi inayowakilisha asilimia 83.78 ya waliotuma maombi. Kwa upande mwingine, ni wanawake sita pekee walitaka kazi hiyo, idadi inayowakilisha asilimia 16.22 ya maombi tuliyopokea kwa nafasi hiyo,” Kasisi Makanda akasema kwenye taarifa.
“Na kati ya watu 37 walioomba nafasi hiyo ya IEBC watatu ni watu wanaoishi na ulemavu (PLWD),” akaongeza.
Kulingana na Kasisi Makanda, jumla ya Wakenya 1, 333 walituma maombi kutaka kujaza nafasi sita za makamishna wa IEBC.
“Kati ya hawa, Wakenya 237 (asilimia 17.77) ni wanawake, 1078 (sawa na asilimia 80.87) ni wanaume Wakenya 18 (asilimia 1.35) hawakuandamanisha vitambulisho vyao vya kitaifa na stakabadhi zao za maombi,” akaeleza.
Kasisi Makanda alisema idadi jumla ya maombi yaliyopokewa na jopo hilo la wanachama tisa, kufikia Februari 15, 2025 ilikuwa 1, 848.
“Tangu wakati huo, tumekuwa tukichambua kwa makini maombi hayo yaliyotumwa kwa njia ya kawaida na barua pepe,” akaeleza.
Kasisi Makanda alitangaza kuwa orodha kamili ya Wakenya wote waliotuma maombi kwa nafasi za mwenyekiti na makamishna wa IEBC itachapishwa katika magazeti mawili makuu nchini Machi 6, 2025.
Aidha, orodha hiyo itachapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali na tovuti ya Bunge.
“Baada ya kuchapishwa kwa orodha hiyo ndefu, Jopo la Uteuzi litaanza mchakato wa kuandaa orodha fupi ya watakaoalikwa kwa mahojiano. Orodha hiyo fupi itachapishwa magazetini, kwenye Gazeti rasmi la Serikali na tovuti ya Bunge,” Kasisi Makanda akaeleza.
Mwenyekiti huyo, kwa mara nyingine, aliwahakikishia Wakenya kwamba jopo lake litatekeleza majukumu yake ndani ya muda wa siku 90 kulingana na hitaji la Sheria ya IEBC ya 2024.