Habari za Kitaifa

Maraga: Serikali ya sasa haipeleki Kenya popote, nina uwezo wa kunyorosha mambo

Na NDUBI MOTURI March 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAJI Mkuu wa zamani David Maraga ameahidi kunyoosha nchi hii na kuirejesha katika mkondo wa utawala bora iwapo Wakenya atamchagua kama rais mwaka wa 2027.

Bw Maraga Alhamisi alisema atapambana na mafisadi ili kuhakikisha katiba inaheshimiwa na watu wote.

Alidai kuwa uongozi wa sasa wa Rais William Ruto haupeleki taifa popote kwa sababu kuna wizi uliokithiri na walio serikalini wanajali tu maslahi yao ya kibinafsi.

“Unapewa rasilimali kushughulikia maslahi ya watu lakini unazinyakua zote. Sasa unaanza kuzungumza kwa lugha ya kuchanganya ukifikiria kuwa baadhi yetu hatukuenda shule,” akasema Bw Maraga.

“Ukweli ni kuwa donda ndugu nchini na mataifa ya Afrika ni ufisadi. Tukifaulu tu kumaliza ufisadi, hatutakuwa na shida zozote. Kama nitapewa nafasi ya kuongoza nchi hii, nitahakikisha kila mtu anatii sheria,” akaongeza.

Alikuwa akiongea kwenye mdahalo na raia wakati wa tamasha ya siku mbili ya vijana jijini Nairobi.

Alikuwa akiwajibu vijana ambao walitaka kufahamu maoni yake kuhusu demokrasia, sheria na suluhu kwa matatizo ya nchi.

Japo kumekuwa na madai kuwa Bw Maraga anapanga kuwania urais, hakulibainisha hilo akisema kuwa anafuatilia na kushiriki vilivyo siasa za nchi.

Alisema bado anasikiliza sauti za vijana na masuala yanayowasibu kabla ya kuamua iwapo atawania urais mnamo 2027 au la.

“Nawauliza, ni kiongozi yupi mnayemtaka kabla ya kuniuliza iwapo nitakuwa debeni. Mnataka nani awanie urais? Bado nafikiria na pia mniambie ni aina gani ya viongozi mnawataka?

“Ni masuala gani yanayohusu raia ambayo mnataka yashughulikiwe? Kwa sasa huu ni mjadala wa kisiasa ambao tunashiriki na tunalenga kuona kile ambacho kitafanyika,” akaongeza.

Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga akishiriki densi na vijana wa Gen Z wakati wa hafla ya The People Dialogue Festival (PDF), Machi 6, 2025. Picha|Francis Nderitu

Bw Maraga amejizolea sifa kedekede kama mpiganiaji wa haki na masuala ya uongozi.

Hasa amekuwa akipigania mageuzi ya kitaasisi kusaidia kupambana na ufisadi.

Alipokuwa jaji mkuu, aliwaongoza majaji wa mahakama hiyo kufuta uchaguzi mkuu wa Agosti 2017 kutokana na udanganyifu na wizi wa kura.

Hii ilikuwa mara ya kwanza ambapo mahakama ilifuta uchaguzi wa urais barani Afrika na kuashiria uhuru wa korti tangu uhuru upatikane.

Mnamo 2020, Bw Maraga alimshauri aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kuvunja bunge kwa kukosa kutekeleza sheria ya thuluthi mbili jinsi inavyotakikana kwenye katiba.

Pia alishutumu juhudi zinazoendelea za kuwaondoa majaji wa mahakama ya juu wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome, akisema zinalenga kutimiza tu maslahi ya kisiasa.

“Tatizo ni kuwa tuna watu ambao wanaibuka na madai yasiyo kweli. Soma maombi ya kuwaondoa majaji hao jinsi yalivyowasilisha na yaliyomo kisha uone mahali ambapo tatizo linatokea,” akasema.

“Iwapo masuala yaliyoibuliwa kwenye maombi yangewasilishwa kisheria kwenye idara husika, basi hili suala lingepata utatuzi. Ni suala la ukosefu wa uaminifu na kuwasaidia wengine kutimiza ajenda zao za kisiasa,” akasema.

Alisema kuwa wakati ambapo alikuwa jaji mkuu, masuala hayo yalishughulikiwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

“Kama kuna madai ya ufisadi, leta ushahidi. Huwezi kusema tu jaji mkuu anastahili kuondolewa afisini kwa sababu alitoa uamuzi ambao haukubaliani nao,” akasema.

“Watu walikuwa wakiniandikia kuwa wanataka jaji aondolewe afisini kwa sababu ametoa uamuzi usiowapendeza. Nilikuwa nawaambia waende katika mahakama ya rufaa,” akasema.

Majaji wa mahakama ya juu wanakodolewa macho na maombi ya kuondolewa afisini baada ya kutoa uamuzi wa kumzima wakili Ahmednasir Abdullahi kuwakilisha wateja wake kwenye mahakama hiyo.

Hii ilitokana na hatua ya Bw Abdullahi kuwakashifu Bi Koome na wenzake kwenye mitandao kuhusu jinsi ambavyo walivyokuwa wakiendesha idara ya mahakama.

Maombi hayo yamewasilishwa na mawakili Nelson Havi na Christopher Rosana.