Michezo

Lionesses ndaaaani nusu-fainali ya Cape Town Challenger, japo kwa jasho

Na GEOFFREY ANENE March 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KENYA Lionesses wamejitosa nusu-fainali ya duru ya pili ya mashindano ya raga za wachezaji saba ya Challenger Series, japo kwa jasho jijini Cape Town nchini Afrika Kusini, Ijumaa.

Lionesses wamemaliza juu ya Kundi A baada ya kupepeta Uganda 10-5 na Ubelgiji 17-5. Kenya itakabana koo na Colombia katika nusu-fainali hapo Jumamosi, Machi 8.

Vipusa wa kocha Dennis Mwanja walizamisha Ubelgiji katika mechi ya kwanza kupitia miguso mitatu ya nahodha Grace Okulu na mkwaju kutoka kwa Sinaida Nyachio.

Lionesses, ambao walishinda duru ya kwanza jijini humo mnamo Machi 2, walitolewa kijasho na Uganda kabla kuwashinda katika muda wa ziada mechi ya pili.

Lionesses walipoibuka mabingwa wa duru ya kwanza papa hapa jijini Cape Town, Jumapili iliyopita. PICHA | WORLD RUGBY

Okulu aliweka Lionesses kifua mbele baada ya kugusa mpira haraka kufuatia kosa la mchezaji wa Uganda katika kisanduku chao cha mita tano dakika chache Samiya Ayikoru kulishwa kadi ya njano na kukaa nje dakika mbili.

Hata hivyo, Lydia Namabiro alirejesha Uganda kwenye mechi aliposawazisha 5-5 baada ya kumzima Sinaida Mokoya kwenye wingi na kufyatuka hadi kisanduku cha miguso.

Kenya na Uganda zilisalia wachezaji sita kwa dakika mbili baada ya Sheila Chajira na Mayimuna Nassozi kulishwa kadi ya njano dakika ya 11 na 12, mtawalia.

Nassozi alionyesha kadi nyekundu dakika ya 17, lakini bado Kenya ilihitaji kujituma zaidi ya kawaida kupachika goli la ushindi kupitia kwa Chajira aliyetumia nguvu kutoka ndani ya kisanduku cha mita tano cha Uganda.

Ngangari

Ushindi huo uliwezesha Wakenya kumaliza juu ya kundi. Uganda waliingia mechi dhidi ya Kenya wakiwa kileleni baada ya kulaza Ubelgiji 22-7 kupitia miguso ya Peace Lekuru (miwili), Grace Auma na Janati Nandudu na mkwaju wa Nassozi. Abigael Bokonda alifunga mguso wa Ubelgiji ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Femke Soens.

Mataifa 12 yanashiriki mashindano haya. Yalitiwa katika makundi manne ya timu tatu tatu ambapo washindi wa makundi – Kenya (Kundi A), Czech (Kundi B), Afrika Kusini (Kundi C) na Colombia (Kundi D) walifuzu kushiriki nusu-fainali.

Timu nane-bora kutoka duru hizi mbili za kwanza zitaingia duru ya tatu mjini Krakow, Poland mnamo Aprili 11-12 kupigania kumaliza nne-bora ili kupata fursa ya kulimana na timu nne za mwisho za Raga za Dunia 2024-2025 hapo Mei mjini Los Angeles, Amerika. Washindi jijini Los Angeles wataingia Raga za Dunia 2025-2026.