Shambulizi la mpakani Turkana: Miili 3 imepatikana, watu 38 bado wametoweka
MIILI mitatu imepatikana kufikia sasa kwenye Ziwa Turkana kufuatia shambulizi lililotekelezwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Dassenech kutoka nchi jirani ya Ethiopia dhidi ya wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara wa Kenya.
Shambulizi hilo la Februari 22, 2025 lilitekelezwa dhidi ya vijiji vya mpakani vya Lotiira na Lopeimukat huko Todonyang’, Kaunti ya Turkana.
Familia zilizoathiriwa ziliripoti kuwa zaidi ya watu 40 hawajulikani waliko tangu shambulizi hilo. Pia boti 47, nyavu na zana 556 za uvuvi, pikipiki moja na bunduki mbili za askari wa akiba hazijapatikana.

“Miili mitatu imepatikana kufikia sasa pamoja na boti tisa na nyavu 122. Watu 38 bado hawajulikani walipo japo msako unaendelea. Tuko na matumaini makubwa kwamba tutawapata watu hao na pia mashua na nyavu,” alisema Naibu Kamishna wa Kaunti ya Turkana Kaskazini George Orina.
Miili miwili ya kwanza ilipatikana siku nne baada ya shambulizi huku mwili wa tatu ukitolewa ziwani siku ya nane baada ya Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) kuzidisha shughuli za uokoaji.
Mratibu wa shirika hilo Kaunti ya Turkana, Rukia Abubakar, alisema wanaendelea na shughuli hizo na kwamba hawajapata miili zaidi au manusura.
“Kwa usaidizi wa mamlaka za usalama kutoka Kenya na Ethiopia, Walinzi wa Pwani ya Kenya na maafisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini tunaendelea na msako,” aliongeza.
Kamishna wa Kanda ya Bonde la Ufa Dkt Abdi Hassan katika mahojiano Ijumaa alisema japo Wakenya 38 bado hawajulikani waliko wengine 66 wamepatikana kufuatia shambulizi hilo la kushtukiza.
Aliongeza kuwa mamlaka za Ethiopia zilisema walipoteza raia wao watatu na wengine 13 wangali wametoweka.