Dimba

Kenya Lionesses wakata kidomodomo cha Afrika Kusini kuibuka tena malkia wa Challenger Series

Na GEOFFREY ANENE March 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA Lionesses walinyamazisha wenyeji Afrika Kusini 17-0 mbele ya mashabiki wao katika fainali ya duru ya pili ya mashindano ya raga ya wachezaji saba ya Challenger Series, jijini Cape Town, Jumamosi.

Lionesses, ambao walipiga Colombia 12-5 katika nusu-fainali baada ya kutoka chini 0-5, waliosha Women Boks kupitia miguso ya Naomi Amuguni, Sharon Auma na Freshia Oduor. Sinaida Nyachio alipachika mkwaju mmoja.

Vipusa wa kocha Dennis Mwanja walilemea Afrika Kusini baada ya kuonyesha ujasiri katika ulinzi, wakizima mashambulizi kadhaa hatari kwa kushinikiza wenyeji hao kufanya makosa.

Freshia Oduor atinga mguso wa Kenya katika mechi hiyo. PICHA | WORLD RUGBY

Lionesses ndio timu pekee imechapa Afrika Kusini katika mashindano hayo. Walibwaga mabingwa hao wa Afrika 17-12 katika nusu-fainali ya duru ya kwanza iliyoandaliwa Machi 1-2 jiini Cape Town kabla kuonyesha hawakubahatisha baada ya kuwanyoa bila maji tena Jumamosi.

Katika fainali ya duru ya kwanza, Lionesses waling’ata Argentina 17-12 katika fainali.

Hapo Jumamosi, Lionesses walianza siku kwa kutolewa kijasho na Colombia kabla ya kuwazima kupitia miguso ya Judith Okumu na Auma. Daniela Alzate alipeleka Colombia mapumzikoni kifua mbele 5-0 kabla ya Kenya kujibu na miguso hiyo katika kipindi cha pili.

Afrika Kusini nao walichabanga Jamhuri ya Czech 21-15 katika nusu-fainali kupitia miguso ya Maria Tshiremba (miwili) na Nadine Roos. Veronika Bolfova, Julie Dolezilova na Tereza Bathova walifungia Czech miguso, lakini hawakupata mikwaju.

Raga za Dunia

Kenya, Afrika Kusini, Argentina, Colombia, Thailand, Czech, Poland na Uganda sasa wamefuzu kushiriki duru ya mwisho ya msimu wa kawaida wa Challenger itakayofanyika Aprili 11-12 mjini Krakow.

Timu nne-bora za Challenger Series zitavaana na nne za mwisho kutoka Raga za Dunia msimu huu wa 2024-2025 ili kuamua timu nne zitakazoshiriki Raga za Dunia muhula ujao wa 2025-2026.