Urafiki wa Ruto, Raila watia ODM kiwewe uchaguzi mdogo wa Magarini
VIONGOZI wa ODM katika Kaunti ya Kilifi, wameomba aliyekuwa Mbunge wa Magarini, Bw Harrison Kombe, aungwe mkono na chama hicho pamoja na Kenya Kwanza katika uchaguzi mdogo.
Bw Kombe alipoteza kiti hicho mnamo Mei mwaka uliopita baada ya mahakama ya juu kushikilia uamuzi kuwa, kulikuwa na udanganyifu na wizi wa kura katika uchaguzi wa 2022 kwa hivyo urudiwe.
Hivi majuzi, Rais William Ruto alisema chama chake cha UDA kitashauriana na ODM kuhusu anayestahili kuungwa mkono katika uchaguzi huo.
Mbunge Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Kilifi, Bi Getrude Mbeyu, alisema viongozi wa ODM katika eneo hilo wakiongozwa na Gavana Gideon Mung’aro watamshawishi Rais kuhakikisha kiti hicho kinasalia katika ODM.
UDA inatarajiwa kumuunga mkono Bw Stanley Kenga, ambaye ndiye aliwasilisha kesi iliyopelekea uchaguzi mdogo kuitishwa. Alikuwa amepata kura 11,925 huku Bw Kombe akiwa na kura 11,946.
Akiwa katika ziara Pwani wiki mbili zilizopita, Rais Ruto alipuuzilia mbali wanaodhani uchaguzi huo mdogo utasambaratisha ushirikiano wake na Bw Odinga.
“Najua kuna mahasidi wanaamini ya kwamba hapa tutachanganyikiwa halafu tufanye mambo tuharibu. Mimi nataka kuwaambia, sisi kama watu ambao tunaamini umoja wa Wakenya, katika mpango wa mapana na marefu yaani ‘broad-based’, hawa tutawachanganya na tutapata mmoja wao na tutatembea na yule ambaye atapatikana,” alisema Rais.