Habari

Kesi ya kutafuta haki kwa Rex Masai yaahirishwa baada ya shahidi muhimu kukosa kuwasili

Na RICHARD MUNGUTI March 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

UCHUNGUZI wa mahakama kubaini kilichosababisha kifo cha Gen Z mwanaharakati Rex Masai Juni 2024 uliahirishwa hadi Alhamisi wiki hii.

Hii ni baada ya afisa wa polisi aliyekuwa msimamizi wa utoaji na matumizi ya silaha kituo cha polisi cha Central kutofika kortini.

Masai aliuawa wakati waandamanaji wa Gen Z waliopinga kutekelezwa kwa Mswada wa Fedha 2024/2025 kupambana na polisi.

Hakimu Mwandamizi Geoffrey Onsarigo alipoingia kortini kuanza kupokea ushahidi, kiongozi wa mashtaka Bi Gikui Gichuhi aliomba uchunguzi uahirishwe kwa vile shahidi Fredrick Ole Tepes hakufika kortini.

Ole Tepes ndiye alikuwa msimamizi wa sehemu ya kuhifadhi silaha katika kituo cha polisi cha Central wakati Rex Masai aliuawa.

Inadaiwa Masai aliuawa na afisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Central.

Ole Tepes alikuwa ameorodhesha kutoa ushahidi wake Jumatatu Machi 10 lakini hakufika kortini.

Ilibidi uchunguzi huo uahirishwe hadi Alhamisi kuwezesha Ole Tepes kufika kortini.

Mbali na Ole Tepes, kulikuwa na shahidi mwingine lakini hangetoa ushahidi hadi afisa huyu wa polisi atoe ushahidi kwanza. Ushahidi wa ole Tepesi ndio msingi wa uchunguzi huu.

Masai aliuawa mnamo Juni 24, 2024 Gen Z walipoongoza maandamano ya kupinga serikali ya William Ruto na kushinikiza ang’atuke mamlakani.

Wakili David Mwangi Chege anayewakilisha familia ya Rex Masai aliambia mahakama kesi hiyo itasikizwa hadi tamati na haki kwa marehemu ipatikane.

Bw Chege alieleza mahakama kwamba tukio hilo la polisi kuwafyatulia risasi Gen Z ambao hawakuwa wamejihami kwa silaha lilikuwa la kusikitisha na sharti waliohusika wapambane na makali ya sheria.

“Tutahakikisha kwamba hakuna afisa wa polisi atakayeua mtu ambaye hana silaha. Kesi hii ndiyo itakuwa msingi wa hilo,” Bw Chege alisema.

Chama cha wanasheria nchini LSK kimemteua Bw Chege kuwajilisha familia ya Rex Masai katika uchunguzi huo.