Majangili wageuza tena Baragoi kuwa bonde la damu
WIMBI la mauaji ambalo lilikuwa likishuhudiwa Baragoi, Kaunti ya Samburu limerejea tena baada ya zaidi ya watu 16 kufa chini ya miezi miwili kwenye visa vipya vya ujangili na wizi wa kimabavu.
Baragoi, kwa sasa inakabiliwa na taharuki baada ya majangili kuwaua watu sita jana na kuwajeruhi wengine wanane katika kisa cha hivi punde cha umwagikaji wa damu.
Makali ya uvamizi wa jana yalikuwa dhahiri huku risasi zilizokuwa zimetumika zikitapakaa kote nayo mazingira yakionekana mahame.
Wafugaji katika eneo hilo jana walikuwa wameamka kama kawaida bila kufahamu mauti yalikuwa yakibisha hodi kutokana na uvamizi wa kushtukiza wa majangili.
Kwa saa kadhaa wafugaji walikabiliana na majangili hao ambao waliwazidi nguvu na kufaulu kuhepa na mifugo yao. Naibu Kamishina wa Samburu Kaskazini Samwel Mwangi alithibitisha mauti hayo huku akisema polisi wametumwa kurejesha utulivu na kuwasaka majangili hao.
Bw Mwangi alikiri kuwa japo kulikuwa na hatua zilizopigwa, na Baragoi kuanza kuwa eneo salama, uvamizi ambao umekuwa ukishuhudiwa kwa miezi miwili sasa ni dalili kuwa amani ambayo imekuwepo inapotea.
“Hadi sasa tumeondoa miili sita kutoka eneo la tukio. Polisi wamefika kuzuia vita zaidi na kuwaandama wavamizi,” Bw Mwangi akaeleza Taifa Leo jana.
“Tumetuma kikosi cha kupambana na wezi wa mifugo (ASTU) na polisi wa akiba. Wavamizi waliojihami vikali walifika eneo la Kilepoi, wakafyatua risasi na kuondoka na mifugo ambayo idadi yao haijulikani,” akaongeza.
Waliojeruhiwa walikimbizwa hadi hospitali ya Baragoi na Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Samburu ili watibiwe huku maafisa wa usalama wakiendelea kutathmini hali ya usalama eneo hilo.
Miili ilipelekwa katika mava ya hospitali ya rufaa ya kaunti mjini Maralal.
Jana, taharuki ilikuwa dhahiri wakazi wakihofia uvamizi mwingine wa kulipiza kisasi ungetokea.
Baada ya miaka miwili ya utulivu, Samburu Kaskazini ambako jamii za Wasamburu na Waturkana zinaishi imekumbwa na utovu wa usalama ambao ulishuhudiwa kwa karibu miaka 30.
Mnamo Februari 27, watu wawili waliuawa kwa risasi na wengine 10 kujeruhiwa katika shambulio la barabarani Maralal-Baragoi, eneo la Mbukoi, Samburu Kaskazini.
Mnamo Machi 9, wezi walimuua Joshua Mark Ndwiga aliyekuwa mfanyabiashara mjini Wamba, Samburu Mashariki. Alikufa papo hapo huku wanawe wawili wakiachwa na majeraha ya risasi.
Mashahidi wanasema kuwa wavamizi hao waliingia katika duka la Bw Ndwiga kama wateja kabla ya kutoa silaha zao na kumuua. Wanawe wawili wanaendelea kutibiwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ambako mwili wa raia mwingine aliyeuawa pia upo.
Polisi wamesema kuwa bado hawajabaini sababu ya kufanyika kwa uvamizi huo na bado wanawaandama washukiwa ili kusaka haki kwa familia ya marehemu.
Ukosefu wa usalama jana ulisababisha maandamano mjini Baragoi, raia wakitoa wito kwa serikali izidishe juhudi za kuwalinda.
Jumatatu, wakazi wa Wamba pia walimiminika barabarani kulalamikia mauaji ya marehemu Ndwiga na kutaka familia yake ipate haki.
Wakiwa na hasira wenyeji waliwasha moto kwenye magurudumu na kuimba nyimbo za kukashifu serikali kwa kutowahakikishia usalama wao.
“Tunaishi kwa hofu na usiku unapotimia, majangili hutuua na hakuna chochote ambacho kinafanyika,” akasema Samwel Lempirikany ambaye alikuwa kati ya waliokuwa wakiandamana.
Wakazi sasa wanalalamika kuwa kuna magenge yaliyojipanga na majangili ambao wanawavamia na kuwazidi ujanja maafisa wa usalama. Baadhi yao wamekuwa wakilenga supamaketi na wafanyabiashara wanaouza bidhaa nyingi.
“Wanakuja wakiwa wamejihami vikali na kwenye makundi huku wakiwa wanajua nini hasa wanataka. Mara nyingi wamejifunika kwa mashuka na hata hupita vizuizi vya polisi,” akasema mfanyabiashara Mohammed Wassar ambaye walimwibia mali ya Sh300,000, duka lake lilipovamiwa eneo la Kisima wiki hii.
Visa vya uvamizi ambapo majangili huelekezea wafanyabiashara bunduki na kuwapora vimekithiri sana katika miji ya Wamba, Maralal, Kisima na Suguta Mar Mar.
Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda alilaumu maafisa wa usalama kwa kuzembea kazini na kushindwa kupambana na wahalifu.
“Polisi waongeze doria kuhakikisha kuna usalama wa wafanyabiashara,” akasema Bi Lesuuda.
Kamishina wa Samburu John Cheruiyot naye alisema sasa wamezidisha doria kupambana na uhalifu huo. Alisikitika kuwa wafanyabiashara wanamiminiwa risasi au kuelekezewa mtutu wa bunduki na kuuawa kinyama.