Makala

Genge lilivyoanzisha seli haramu ambako huzuilia na kutesa wakazi bila polisi kujua

Na OUKO OKUSAH March 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wanaoishi viungani mwa mji wa Kakamega wamekuwa wakihangaishwa na genge hatari ambalo lilifungua seli haramu na limekuwa likiwanyaka, kuwazuilia na kuwaangushia kichapo kikali.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, wakazi hao walisimulia jinsi baadhi yao walikuwa wakipigwa na kuachwa na majeraha huku wengi wao wakihofia kuzungumzia madhila yao ili wasivamiwe tena.

Mnamo Machi 5 Lilian Chemayo alivamiwa na wanaume wenye miraba minne na wanawake waliokula vizuri. Walimuuliza kwa nini mwanawe na hata kabla ajibu, mwanaume mmoja alimwaangusha chini kisha akaamrisha wanawake wamtandike.

“Walichukua simu yangu, pesa na bidhaa nyingine,” akasema Bi Chemayo akidondokwa na machozi.

Kundi hilo kisha lilimpeleka Bi Chemayo kwenye seli ya karibu likampa kipigo zaidi kisha likamfungia.

“Kifua changu, mgongo na mikono yangu ilikuwa na majeraha. Nilikuwa natokwa na damu sehemu zote za mwili kutokana na majeraha mabaya,” akaongeza Bi Chemayo.

Aliachiliwa tu baada ya kulipa Sh300.

Mambo si tofauti kwa Mildred Ayuma ambaye alibebwa juu juu kutoka mlango wake mnamo Machi 6 kisha akapelekwa kwenye seli bila kupewa ufafanuzi wowote.

“Nilipofikishwa seli, niliwapata ‘mahabusu’ wengine wakicharazwa viboko. Hawakutuambia kwa nini tulikuwa tukizuiliwa kwa kuwa walifungua mlango wakatupiga kisha kutoka.

“Walirejea na kuendeleza mtindo huo wa kutupiga kwa siku tatu mfululizo ambapo nilizuiliwa,” akasema Bi Ayuma.

Alieleza kuwa seli ilikuwa imejaa giza, ilikuwa na kuta ambazo zimepasuka na kulikuwa na mitungi miwili ya maji kisha ndoo ambayo ilitumika kuenda haja.

Lilian Imali naye anakumbuka kuwa mnamo Machi 7, alikuwa akioga genge hilo lilipofika kwenye mlango wa bafu na kumtaka aandamane nao.

“Juhudi zangu za kuwataka waniambie makosa yangu ziliangukia pua. Waliniambia ningejua sababu baadaye,” akasema Bi Imali ambaye aliingizwa selini humo saa 10 jioni.

Alimpata Bi Ayuma na watu wengi saba waliokuwa wakizuiliwa wakiwemo wanaume ambao walikuwa wakilia kutokana na maumivu.

“Saa sita usiku, walianza kutupiga. Walinicharaza viboko hadi mapaja yangu yakafa ganzi. Walitupa ugali na sukumawiki jioni pekee lakini hatukuruhusiwa kuenda nje,” akasema na kufichua aliachiliwa pia baada ya kulipa Sh300.

Kwa muda wa wiki moja, genge hilo lilifungua seli hiyo huku likiwanyanyasa na kuwapora watu ambao walifikiria wamevunja sheria bila kuelezwa sababu.

Bi Jacklyne Musa ambaye nyumba yake ni karibu na seli hiyo bandia alisema aliwauliza wanachama wa genge hilo kwa nini walikuwa wakiwazuilia na kuwatesa watu lakini akaonywa.

“Waliniambia hata mimi watanizuilia nikiendelea kuwauliza maswali na sitatoka nikiwa hai. Hiyo siku walikuwa wakiwazuilia watu watano,” akasema.

Alipowauliza kwa mara nyingine aliposhuhudia watu watatu wakipigwa, kutolewa nguo kisha kuachwa uchi, walimwaambia walilenga kumaliza ulevi na uuzaji wa mihadarati.

Wenyeji wanasema kuwa genge hilo lilitumia msingi kwamba mitaa ya mabanda huwa na visa vya matumizi na uuzaji wa mihadarati, pombe haramu, dhuluma dhidi ya watoto kuendeleza shughuli zao za kikatili.

Naibu Chifu Isaac Ayumba alifahamishwa kuhusu vitendo hivyo mnamo Jumanne na akamfikia mzee wa kijiji kisha wakafahamisha polisi na washukiwa sita wakakamatwa.

Wakati wa uvamizi uliolenga genge hilo, watu tisa waliokuwa wakizuiliwa waliachiliwa huru wengine wakiwa bado na majeraha ya kupigwa.

Polisi pia walipata rungu, viboko na kamba zilizokuwa zikitumika kwenye seli.

“Polisi wanawasaka wanachama wa genge hilo na wale ambao walipigwa na kuzuiliwa pia tunawaomba wajitokeze kuandikisha taarifa,” akasema Bw Ayumba.

“Pia tumeagiza mmiliki wa nyumba ambayo seli ilikuwa atoe mwanga zaidi kuhusu unyama huu,” akaongeza.

Mkazi Zamzam Swale alisema wakazi waliamua kuteseka bila kuzungumza kwa sababu walihofia wanachama wa genge hilo wangewadhuru na hata kuwaua.